January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mrithi wa Kinana CCM kujulikana katika Mkutano Mkuu wa Jan 18/19

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kufanya Mkutano Mkuu Januari 18 na 19, mwaka huu, jijini Dodoma, ambapo ajenda kuu zitajumuisha uchaguzi wa kumpata Makamu Mwenyekiti mpya wa chama hicho kwa upande wa Bara.

Uchaguzi huu unafanyika kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana, mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 7, 2025, Jijini Dodoma, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA. Amos Makalla, amesema mkutano mkuu huo utafunguliwa na vikao vya Kamati Kuu ya CCM, na kisha kufuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kitakachofanyika Januari 16, mwaka huu.

Makalla aliongeza kuwa ajenda nyingine za mkutano mkuu huo zitajumuisha kupokea taarifa za utekelezaji wa kazi za chama katika kipindi cha 2020-2025, pamoja na taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mkutano huu mkuu unatarajiwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa chama hicho, huku akisubiriwa kwa hamu uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti mpya ambaye atachukua nafasi iliyoachwa na Kinana.