January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mrembo afariki dunia akitengeneza shepu

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MREMBO maarufu Nchini Nigeria, kwenye mitandao ya kijamii (sosholaiti), Amelia Pounds anaripotiwa kufariki dunia nchini India alipokuwa akifanyiwa upasuaji wa liposuction, ambao ulimwendea vibaya.

Liposuction ni sajari au upasuaji wa kupunguza mafuta katika sehemu ya utumbo wa chini.

Ni upasuaji wa kuongeza urembo ambao umekumbatiwa na warembo na mastaa wengi ambao wanathamini mionekano yao, wengi wakiwa wale wanaotaka kuwa na viuno laini na vyembamba kama nyigu.

Katika video ambayo imekuwa ikisambazwa mitandaoni, Amelia alionekana amezima kabisa na mwili wake kugeuka gogo lisiloweza kujisogeza.

Imeripotiwa kuwa aliaga dunia Ijumaa iliyopita asubuhi, Oktoba 7, mwaka huu, ingawa haijulikani ni nini kilisababisha matatizo hayo, inasemekana alikata roho wakati akifanyiwa upasuaji hospitalini.

Kifo chake kinatokea siku chache tu baada ya mwanamama maarufu nchini Kenya, Vera Sidika kusimulia kwamba alinusurika kifo kutokana na upasuaji wake wa kuongeza makalio.