November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mramba:Bomba Mafuta Ohima wafikia pazuri

Na Penina Malundo ,Timesmajira

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba amesema mradi bomba la mafuta la ECOP kutoka Ohima nchini Uganda Hadi Chongoleani Tanga,mpaka sasa mradi huo umeshafanyiwa usanifu na ulipaji fidia kwa baadhi ya watu.

Akizungumza hayo jana Mramba katika banda la Shirika la Maendeleo Petroli Tanzania(TPDC) alipotembelea katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es salaam,alisema tathimini ya jumla ya mradi huo hadi sasa umefikia asilimia 30.

Amesema tayari baadhi ya watu wamelipwa fidia zao na wachache waliobakia ambao wana mambo ya mirathi nao wanaendelea kulipwa.

“Mpaka mwakani mwishoni mradi utakuwa umekamilika kulingana na ratiba ya mradi na hivi ninavyozungumza tayari kilomita zaidi ya 600 za mabomba zimetandikwa chini mambo yanaenda vizuri,”amesema.

Aidha amesema serikali inatarajia kuongeza vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari kutoka viwili hadi vituo zaidi ya 30 vilivyopo mkoani Dar es Salaam.

Amesema ifikapo mwaka 2025 vituo hivyo vitawawezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.Mramba alisema TPDC imejiongeza pamoja na kujenga vituo kwa mfumo wa kawaida uliozoeleka pia wataleta magari ambayo yatauza gesi huku yanatembea.

Aidha amesema mpaka mwakani kutakuwa na magari mengi yanaegesha huku akitolea mfano kuwa siku fulani wakiamua kuegesha Mwananyamala itakaa hapo na wateja wa maeneo hayo wataendana magari yao ili wajaziwe gesi.

“Natoa wito kwa TPDC kuhakikisha mnatanua wigo wa usambazaji wa gesi asilia kwa kushirikiana na sekta binafsi lengo ikiwa ni kuhakikisha gesi asilia inawafikia Watanzania wengi zaidi kwa haraka.