Joyce Kasiki
HIVI karibuni,Shirika linaloangazia Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (CiC) kupitia mradi wake wa Watoto Wetu Tunu Yetu limefanikiwa kufikia wilaya zote za mkoa wa Dodoma kwa kutoa mafunzo ya uboreshaji ,ufundishaji na ujifunzaji wa darasa la elimu ya awali kwa lengo la kuhakikisha watoto wa darasa hilo wanaandaliwa vyema kuingia darasa la kwanza wakiwa wanajua kusoma,kuandika na kuhesabu.
Wilaya hizo ni Kongwa,Chamwino,Dodoma,Mpwapwa ,Bahi,Kondoa Mji,Wilaya ya Kondoa na Chemba .
Mratibu wa Mradi huo kwa mkoa wa Dodoma Frank Samson anaeleza mafanikio ya mradi huo kuwa ni pamoja na kusaidia ukarabati ,uandaaji wa madarasa changamshi na ya kuvutia kwa watoto wa darasa la Elimu ya Awali Katika shule 232,ukarabati mdogo wa vyumba 232 , michoro ya ndani na nje ya darasa na hivyo kuchochea ujifunzaji kwa vitendo na michezo kwa watoto .
Pia Mradi umeweza kujenga na kumalizia vyumba 26 katika wilaya hizo ,umetoa mafunzo ya kujenga uwezo wa usimamizi ,utoaji na uratibu wa elimu bora ya awali kwa walimu wakuu 232, maafisa Elimu kata 232, walimu darasa la Elimu ya Awali 232 na walimu wa taaluma 58,
Anabainisha kuwa ,Mradi umesaidia kufunga mifumo ya maji katika shule 41 na kuunganisha maji ya bomba Katika shule 10 , umetoa vifaa vya kusaidia ufundishaji na ujifunzaji wa walimu kwa watoto na walimu ,maturubai na vifaa vingine ili kuchochea ujifunzaji wa watoto na kuhakikisha wanaomuda kusoma, kuandika na kuhesabu kwa hatua za awali lakini pia umeandaa vitabu vitakavyowawezesha kujisomea nyumbani.
Anasema,mwaka 2023, mradi umeanza kutekelezwa mkoa mzima wa Dodoma, ukilenga kuzifikia shule zote karibu 800 ambapo tayari umeshatoa mafunzo kwa walimu wa darasa la elimu ya awali katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma yanayolenga kuwafanya kuwa walimu bora wa Elimu ya Awali, kuongeza umahiri wa ufundishaji, kutengeneza na kuendeleza mazingira ya kujifunza kwa kutumia vifaa vilivyopo kwenye mazingira ili kuchochea utoaji wa Elimu bora ya Awali.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya walimu wilayani Kondoa Mkurugenzi wa CiC Craig Ferla anasema,Mkoa wa Dodoma unapaswa kuwa mfano na watu wengine waende kujifunza namna ya elimu ya darasa la awali inavyotolewa huku akisema ni imani ya Shirika hilo kama elimu ya awali ikinawiri mkoani humo inaweza ikawa chachu katika ubora wa elimu ya awali na mikoa mingine.
“Na ndiyo ndoto na imani yetu,tukiona mageuzi hapa Dodoma ,tunaamini inaweza ikawa na mchango mkubwa katika kuleta ubora wa elimu ya awali nchi nzima ,kwa hiyo tupo hapa kimkakati,awamu ya kwanza tumemaliza ya kushirikiana na Serikali katika wilaya zetu za Kongwa na Chamwino kwa kufikia shule zaidi ya 230 na tumeona kwamba inawezekana ,sasa tumeingia mkoa mzima wa Dodoma,pamoja na changamoto zilizopo lakini mkidhamiria inawezekana kabisa.” anasema Craig
Kwa mujibu wa Sensa ya 2022 asilimia 29 ya watanzania wana umri wa miaka 0-9 kwa maana ya umri unaohitaji kuzingatiwa katika malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ili kuhakikisha mtoto anakua hadi kufikia utimilifu wake na hivyo Taifa kuwa na nguvukazi yenye tija katika kutafakari na kufanya maamuzi na hatimaye kufikia maendeleo tarajiwa ,lakini pia hicho ndiyo kizazi ambacho kitasukuma maendeleo yaTanzania kwenye dira yetu ya 2050 .
“Kuna ushahidi tosha kwamba kama tungeweza kuwekeza kwa watoto wetu wadogo kwenye kile kipindi ambapo ubongo wao ndiyo hasa unakua kwa asilimia 90,ukweli ni kwamba ndiyo tunaandaa Taifa la kesho na kizazi ambacho kitakuwa kinatuletea maendeleo.”anasema Craig
Vile vile anasema robo tatu ya Sensa ya watu na Makazi ya 2022 kulikuwa na maswali matatu ambayo yalikuwa yanahusu masuala mazima ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za kwanza kuwa na kiashiria kwenye hiyo Sensa ikiambatana na tafiti kwenye masuala ya afya na maendeleo cha ECDi 2030.
“Hiki ni kiashiria ambacho kinahusu masuala mazima ya watoto wadogo na kuwezesha Tanzania ku-‘report’ kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu ya kidunia ambapo kwenye hicho kiashiria kinaonyesha kuwa asilimia 47 ya watoto wetu wenye umri wa miaka mitano wana makuzi sahihi kwa maana kwamba nusu ya watoto wetu hawajafikia utimilifu wao yaani hawana makuzi sahihi suala ambalo ni hatari kwa Taifa katika kupoteza nguvukazi yake,
“Sisi tunaichukulia hii kama ni fursa ya kipekee ,kama karibu theluthi moja ya watanzania wote wana umri wa miaka 0-9 tukiwekeza kwao kwa hali na mali kwa hiki kizazi kijacho tunaweza kutumia dirisha hilo kwa Tanzania kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo kwa kizazi kijacho maana hawa watoto wote baada ya miaka kadhaa ndiyo watakuja kuwa rasilimali kubwa ya Taifa kwenye kusukuma maendeleo,
“Kwa hiyo inabidi tutumie dirisha hilo kwa sababu baada ya vizazi viwili hivi tutakuja kujikuta kwamba watanzania wengi zaidi wapo kwenye umri wa kustaafu, na nafasi ya kuwekeza kwa watoto na kuona kwamba tunapiga hatua kubwa kwenye maendeleo ya kipekee ndiyo sasa”
Craig anasema,upo ushahidi kwamba ukiwekeza kwenye elimu ya awali watoto wanakua na utayari wa kuingia shule na wanafanikiwa kwa kiwango kikubwa kwenye Kusoma,Kuhebu na Kuandika na ambazo humwezesha mtoto kupata mafanikio katika safari nzima ya elimu,kwenye maisha, kiuchumi na kijamii .
Aidha anasema,CiC inatambua juhudi kubwa za serikali ya awamu ya sita kwenye kuwekeza kwenye elimu ya awali kwa kuiingiza kwenye Sera ya Elimu ya Msingi na kuwa sehemu ya mpango wa elimu bila malipo.
“Tunajua kwamba kuna nguvu kubwa katika suala la miundombinu kwenye elimu ya awali na vile vile tunajua kwamba kwa pamoja tunashirikiana katika suala la walimu wa awali na bado tuna safari..,kwa upande wa CiC tunashirikiana kwa karibu na serikali na wizara za kisekta ili kutimiza ndoto za kuwekeza kwenye darasa la elimu ya awali na ndipo tutaweza kubadli safari nzima ya elimu ya watoto wetu”
Mgeni rasmi katika mafunzo hayo Dkt.Emson Mgogo kutoka Idara ya Usimamizi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI ,Seksheni ya Elimu Awali na Elimu Msingi anasema kinachofanywa na CiC ni sehemu ya kuiunga serikali mkono katika jitihada zake za kuboresha elimu hususan elimu ya awali.Anatumia nafasi hiyo kuwataka viongozi wote waliohudhuria mafunzo hayo ,kwenda kusimamia vizuri mradi huo.
Anasema mbali na kwenda kuandaa madarasa yanayoongea pia wahakikishe madarasa hayo yanatumika kikamilifu ili kuwajengea uwezo watoto wa kumudu mahiri za kusoma kuandika na kuhesabu huku akiwataka wadhibiti Ubora wa shule ngazi zote kwenda kutimiza wajibu wake kikamilifu ili kuleta matokeo chanya yanayotarajiwa katika sekta ya elimu.
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Elimu mkoa wa Dodoma Borasa Chibura amelishukuru la CiC kupeleka mradi wa Watoto Wetu Tunu Yetu katika mkoa wa Dodoma huku akisema Shirika hilo limeuheshimisha mkoa huo huku akisema kuwa mkoa wa Dodoma sasa unaenda kuwa walimu mahiri wa darasa la elimu ya awali ambao wataenda kufundisha vizuri mahiri zote kwa watoto wa elimu ya awali .
“Niwahakikishie mkoa wa Dodoma unaenda kuwa kitovu cha watu kuja kujifunza namna gani elimu ya awali inapaswa kuendeshwa.”
Mwalimu wa darasa la elimu ya awali katika shule ya Msingi Igoji Kaskazini Wilayani Mpwapwa Frank Masamale anasema,amefurahishwa na CiC kutambua umuhimu wa elimu ya awali huku akiomba mafunzo hayo yawe endelevu na walimu wote wa darasa la awali nchini wapate elimu hiyo kwa mustakabali wa Taifa.
Afisa Elimu Kata,Kata ya Lumuma Wilayani Mpwapwa Batlet Mfugale anasema ,watoto wa darasa la elimu ya awali wanahitaji kufundishwa kwa ukaribu zaidi ili waweze kujifunza na kujua kusoma kuandika na kuhesabu ili wawe wazuri zaidi wanapofika madarasa ya juu.
“Kama mradi wa Watoto Wetu Tunu Yetu kama ukizingatiwa,kusimamiwa na watoto wakapata stahili zote zinazotakiwa wataweza kumudu stadi zote tatu watakapokuwa madarasa ya juu kwa sababu elimu awali ndiyo msingi wa watoto wetu.”
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja