January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa upandaji miti kunufaisha Kata tano igunga

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WAKAZI wa Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora wameeleza kufurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na Mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji ya Ziwa Victoria katika kata za Ziba, Ndembezi, Ugaka, Nkinga na Kitangiri ya utunzaji mazingira.

Wakiongea na gazeti hili kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa Wilaya hiyo wamesema wakandarasi wengi hawazingatii sheria za utunzaji mazingira wakati wa kutekeleza miradi wanayopewa licha ya kutakiwa kufanya hivyo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Igumila, kata ya Ziba, Jongo Emanuel alisema hadi sasa wamepewa zaidi ya miche 100 ya miti na Kampuni ya Helpdesk Engineering Tanzania Ltd inayotekeleza mradi wa maji ili kuipanda kijijini hapo.

Alibainisha kuwa utekelezaji miradi ya maji huambatana na ukataji miti na uchimbaji mifereji hivyo kupelekea uharibifu wa mazingira, lakini kampuni hiyo imeanzisha programu ya kugawa miche ya miti ili ipandwe katika kata zote.

‘Tunampongeza Mkandarasi kwa kuanzisha mpango huu wa uhifadhi mazingira katika kata na vijiji vyote vinavyopitiwa na mradi huu, utaratibu huu utasaidia sana kurejesha mazingira yaliyoharibiwa katika hali yake ya kawaida’, alisema.

Diwani wa Kata ya Ndembezi Otto Mayunga alieleza kuwa ukataji wa miti ni adui mkubwa wa mazingira kwani husababisha ardhi kukauka kwa kukosa maji, hivyo mpango huo ulioanzishwa na Mkandarasi unapaswa kuigwa na wadau wote.

Alibainisha serikali imekuwa ikihamasisha kila mtu kabla ya kukata mti apande mti, lakini jamii ikiwemo baadhi ya wakandarasi wamekuwa hawatilii maanani hili hivyo kupelekea uharibifu wa mazingira katika maeneo mengi nchini.

Mkazi wa Kata ya Ugaka, Christina Lazaro alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea zaidi ya sh bil 5.3 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa maji safi na salama kutoka Kata ya Ziba hadi Nkinga.

Aliongeza kuwa licha ya manufaa makubwa yatakayopatikana kupitia mradi huo pia mazingira yataboreshwa kwa kiasi kikubwa kutokana na juhudi kubwa zinazofanwa na Mkandarasi za kugawa miti 100 kwa kila kijiji ili ipandwe.

Naye Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Joseph Mafuru alisema hadi sasa Mkandarasi huyo ameshatoa zaidi ya miche 500 kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo hivyo akawataka wakazi wote wa kata hizo kuchukua miti na kuipanda.

Alisisitiza kuwa uwepo wa miti unalinda ardhi na kila kitu kinachohitajiwa na jamii kinapatikana kwenye ardhi, hivyo ukikata miti utafanya jamii ikose mvua, kuni, hewa safi, ardhi nzuri kwa kilimo na madhara mengine mengi.