January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa umeme wa SGR wakamilika asilimia 99

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Morogoro

MRADI wa miundombinu ya umeme ambao utatumika kuendesha mradi wa treni ya umeme ijulikanayo kama SGR, unaojengwa na Shirika la Umeme TANESCO wenye urefu wa kilometa 159 kuanzia Kinyerezi, jijini Dar es Salaam hadi mkoani Morogoro katika eneo la Kingolwira umekamilika kwa asilimia 99.

Meneja wa Mradi huo kutoka Shirika la Umeme Nchini TANESCO Mhandisi Albano Mahimbo. Picha zote na KVIS Blog

Akizungumza wakati wa ziara ya Wakuu, Wahariri na Wanahabari nchini mapema leo, Meneja wa TANESCO Mradi wa Umeme wa SGR kutoka Kinyerezi hadi Morogoro, Mhandisi Albano Semboe amesema mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100.

Amesema mradi ulianza mwaka 2019 na sasa umefika hatua ya mwisho kabla ya kuwasha umeme. Mradi una jumla ya nguzo za umeme 462, ambapo nguzo zote zimeshasimamishwa na nyaya zote zimeishavutwa.

Semboe aliongeza kwamba kutokana na mradi huo, kwa sasa kinachoendelea ni ukaguzi mdogo ambao unafanyika kabla ya kuweka na kuwasha umeme.

“Kwa sasa kinachoendelea ni ukaguzi mdogo kabla ya kuweka umeme, tumeshaanza na tumekamilisha jana, kinachofuata ni kuunganisha kwenye vituo vya SGR,” amesema Semboe

Wakuu, Wahariri na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wako mkoani Morogoro katika semina ya siku 3 iliyoandaliwa na Shirika la Umeme TANESCO yenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu masuala mbalimbali ya umeme ikiwa ni pamoja na mradi wa Bwawa la Julius Nyerere litakalozalisha umeme wa megawati 2115, ulioko Rufiji, Mkoa wa Pwani.