January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa Ujenzi wa Umeme Rusumo wafikia asilimia 99.6 kukamilika kwake.

Na Penina Malundo, timesmajira

MRADI wa ujenzi wa umeme katika maporomoko ya mto Rusumo mpakani mwa Tanzania ,Rwanda na
Burundi kwa sasa umefikia asilimia 99.6 ya ukamilikaji wake wa kuanza kusambaza umeme katika nchi hizo.

Umeme utakaozalishwa na chanzo hicho cha maji katika maporomoko hayo utakuwa wa megawati
80,ambapo kila nchi ikiwemo Tanzania,Rwanda na Burundi zitaweza kupata megawati 27 kutoka katika chanzo hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni kutoka nchi sita ikiwemo Tanzania,Kenya,Uganda,Rwanda,Kongo
na Burundi,Meneja mradi wa Kanda kutoka Nile Equatorial Lakes Subsidiary Action Program Coordination Unit (NELSAP – CU),Mhandisi Issac Alukwe, amesema umeme utakaozalishwa katika maporomoko haya utaweza kutumiaka kwa nchi tatu kwa usawa kama ulivyokubaliana.

Amesema mradi huu uliopata fedha kutoka Benki ya Duniani kupitia taasisi ya Nile Basin Initiative (NELSAP)kwaajili ya kutumika kwa mradi kwa sasa unakaribia kukamilika na kuweza kuongeza nguvu ya umeme katika nchi hizo tatu.

‘’Kwa nchi ya Tanzania utatumika kwa upande wa Mikoa ya Magharibi na kusini mwa Tanzania huku kwa nchi ya Rwanda utatumika wa upande wa Mashariki na kwa nchi ya Burundi kwa eneo la Bunjumbura,hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhaba wa umeme katika nchi hizi’’anasema

Anasema mradi huu wa umeme wa maji ni mzuri na ni rafiki wa mazingira ukitofautisha na aina nyingine ya umeme na gharama yake ipo chini kwa watumiaji ‘’Huu mradi ni mzuri sana nchi hizi zote tatu zitaweza kunufaika na huu umeme,tunatoa wito kwa nchi nyingine kuja na miradi kama hii ambayo zitaunganisha mikoa katika nchi moja na nyingine na sio kwa umeme pekee hata vitu vingine,’’alisema.

Anasema licha ya kufikia asilimia 99.6 ya ukamilikaji wa mradi huo awali walikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo usumbufu kwa wataalam katika kuvuka mipaka pindi wanavyofanya shughuli zao pamoja na ugonjwa wa covid 19 lakini waliweza kuzitafutia changamoto hizo na kazi kufanyika kwa uhakika.

Kwa Upande wake,Meneja Mradi wa
Rusumo,Mhandisi Aloyce Oduor amesema
umeme wa maji unafaida kubwa kwa watumiaji kuliko aina nyingine ya umeme kutokana na gharama zake kuwa chini.

Oduor amesema mradi huo umeweza kuwasaidia wananchi wa pande zote tatu kunufaika nao kwa kuwapata wataalam wa aina mbalimbali ikiwemo Mafundi Umeme na Mafundi selemara(Cappenter)
wa nchi zote na kufanya kazi kwa usawa.

Mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia makubaliano ya Kiserikali ya nchi za Tanzania,Rwanda na Burundi baada ya kuingia makubaliano rasmi mwaka 2012 na kutoa ajira zaidi ya 1000 kwa nchi zote tatu.

Mradi unatekelezwa chini ya wakandarasi wanne ambapo wawili kutoka China , Kampuni ya
CGCOC Group na Kampuni ya Jiangxi Water & Hydropower construction ambao wamejenga bwawa la maji pamoja na miundombinu mingine na muunganiko wa wakandarasi Andritz Hydro GmbH ya Ujerumani na Kampuni ya Andritz Hydro PVT ya nchini India ambao wanahusika na ufungaji wa mitambo ya kuzalisha na kusambaza Umeme.