November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa Tembo pilipili unavyowasaidia wakulima kufukuza tembo shambani

Na Penina Malundo

UVAMIZI wa Tembo katika mashamba ya wakulima wengi nchini,umekuwa kilio kikubwa kwa wakulima na watu wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa hifadhi kutokana na wanyama hao kuacha kutoka katika maeneo ya hifadhi na kuingia katika maeneo ya makazi ya watu kisha kuvamia mashamba na kufanya uharibifu hususani katika mazao ya chakula,kujeruhi na hata kuua watu.

Hali hii imekuwa ni changamoto kubwa kwa wakazi na wakulima wanaoishi katika maeneo hayo ambapo imefanya kuweza kubuni mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyama hao ili kuweza kulinda uhai wao,mashamba yao pamoja na kuzuia uharibifu unaofanywa na tembo hao pindi wanapoingia shambani na kufanya uharibifu.

Jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na wataalam wa mazingira pamoja na wanyamapori kuhakikisha wanatafuta mbinu za kuwadhibiti tembo kuingia katika makazi ya watu na kufanya uharibifu katika makazi yao na mashamba yaliyokaribu na hifadhi.

Miongoni mwa mbinu ambayo wataalam hao wamekuja nayo ni pamoja na ulimaji wa zao la pilipili katika mashamba yao ambapo inaonekana ni mbinu sahihi inayosaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia kwa wanyama hao kutoharibu mazingira, mazao au kutishia maisha ya binadamu.

Mbinu hii ndiyo imebainika kuwa mbinu sahihi inayosaidia kwa muda mrefu tembo kutoingia katika maeneo yenye shughuli za binadamu na kufanya uharibifu ambapo hutumika kwa njia mbili ikiwemo ya utengenezaji wa tofali la kinyesi cha Tembo au Ng’ombe kisha kuchanganya na pilipili au kutumia Oil chafu,vitambaa vya pamba,kamba za katani ambayo inayochanyanywa na pilipili iliyosagwa kisha kuifunga kama uzio kwenye nguzo za miti iliyozungushwa shambani.

Francis Ndemela,Afisa Miradi ambaye pia ni Afisa Mahusiano wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Tembo Pilipili Program (TPP) ambapo makao makuu yapo Mikumi Mkoani Morogoro, anasema awali wakulima walikuwa wanapata shida mbalimbali katika kukabiliana na tembo wanapoingia katika mashamba yao na kula mazao wanayolima.

Anasema kilio hicho kilikuwa kinasikika hasa kipindi cha mavuno ambapo tembo wakiingia ndani ya shamba hufanya uharibifu mkubwa hali ambayo wakulima huingia kupata hasara kutokana na kupoteza mazao hayo na kupelekea kuishi maisha magumu ya kukosa chakula.

Ndemela anasema taasisi yao kwa kuona uharibifu huo ikaja na mbinu mpya ya kufundisha wakulima hao namna ya kukabiliana na tembo hao kwa mbinu ya pilipili ambayo ni rahisi na gharama nafuu ili tembo wasiendelee kuharibu mazao yao ambao kwa asilimia kubwa yanakuwa katika hatua ya kuyavuna.

”Tumeamua kuja na mradi wa TEMBO PILIPILI kwa lengo la kusaidia wakulima hawa kukabiliana na tembo hawa wanaofanya uharibifu katika mashamba yao,na njia hii inatumika na watu wote wanawake na wanaume na njia rahisi ambayo imekuwa ikiwakimbiza tembo kuingia katika mashamba yanayokuwa karibu na hifadhi za wanyamapori kwani pilipili inamkera tembo kwa kumuwasha,”anasema na kuongeza

”Tunawaelekeza namna ya utumiaji wa pilipili katika kupambana na tembo hao kwa kuwaelekeza kuchukua pilipili ambazo wanazitwanga na kupata unga unga kisha kuchanganya na oil chafu ambayo wanakuja kupaka katika vitambaa vitakavyofungwa kwenye kamba za katani na kuchomekwa katika miti,”anasema.

Anasema njia hii inasaidia kwa kiasi kikubwa kufukuza tembo pindi wasikiapo harufu ya pilipili na oil chafu inawafanya kuwakimbiza wasiweze kusogelea mazao na kufanya uharibifu wowote ule.

‘Mbali ya njia hii pia kunanjia nyingine ambayo uwa tunawafundisha wakulima ni ya kutengeneza tofali la pilipili , yaani kinyesi cha tembo au ng’ombe kisha huchanganywa na pilipili iliyosagwa na kutengeneza tofali ambalo huwekwa katika shamba na kuchomwa moto ambapo moshi wake unapotoa harufu hufanya tembo kutosogea katika eneo hilo,”anasema.

Anasema hadi sasa wameweza kutoa mafunzo hayo kwa wakulima wapatao 3000,katika mikoa mbalimbali yenye vijiji vilivyokaribu na hifadhi za wanyamapori ikiwemo vijiji vilivyopo katika hifadhi ya Mikumi,Ruaha,lake Manyara,Tarangire,Ngorongoro,Bariadi mkoani Simiyu pamoja na Mbuga ya Selous.

”Pilipili inasaidia kwa kiasi kikubwa kufukuza hawa tembo na inasaidia kwa sababu inawasha hivyo tembo watapokuwa wanakuja kuingia katika mashamba ya wakulima wanakutana na harufu hiyo ya pilipili na oili chafu wanaposikia tu wanageuza nyuma na kurudi walipotoka,”anasema na kuongeza

”Tembo mara nyingi wanaingia katika mashamba ya wakulima kipindi ambacho mkulima anaelekea kuvuna,tena wanapenda sana mazao ya chakula wakiingia shambani wanaharibu mazao yote pia wanyama hawa hunusa harufu kwa umbali wa kilometa 20,”anasema.

Anasema wakulima wengi walikua wanabuni mbinu zao za kuwazuia tembo hao kutoingia shambani ikiwemo mbinu ya kupiga kelele ,kupiga madebe au kuchoma moto mipira ya magari kama tairi au viatu ambapo mbinu hizo hazikuweza kusaidia kwa kiasi kikubwa.

”Matarajio yetu kufikia wakulima wengi lengo kuzunguka nchi nzima katika kuwasaidia wakulima hawa wanaoishi pembezoni mwa hifadhi za wanyamapori huku serikali nayo kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuwasaidia ili kuweza kuwalinda wakulima hao na mazao yao,”anasema na kuongeza.’

‘Mradi huu pia unasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza au kuondoa ujangili kwa watu wanaowaua tembo kwa kupata faida zao binafsi,”anasema

Kwa Upande wake Mkulima kutoka kijiji cha Mhenda Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, Blandina Vanali anasema kabla ya wataalamu hao kutoka taasisi ya Tembo Pilipili kufika katika kijiji chao walikuwa wanapata changamoto kubwa ya tembo kuingia katika mashamba yao na kufanya uharibifu.’

‘Utakuta mtu kalima heka yake moja ya mahindi hapo ndo yanakuwa tayari kwaajili ya kuvunwa unaona kundi la tembo linaingia shambani na kuharibu mahindi na wanapoingia wanaharibu kila kitu hawabakizi kitu hata kimoja,”anasema.

Anasema baada ya kutumia njia ya Pilipili na Oili chafu imewasaidia kwa kiasi kikubwa sasa tembo hao kutoingia tena katika mashamba yao na sasa yapata mwaka mmoja hatujaona tembo wakiingia katika mashamba yetu na kufanya uharibifu.Faida nyingine ni kwamba mkulima akilima pilipili kwa wingi anaweza kujipatia kipato cha ziada,hivyo ataweza kulima pilipili ili kufanya uhifadhi na kufanya biashara ya kuuza pilipili au unga wake kwenye viwanda vya chili sauce.

Pia mradi wa tembo pilipili umewasaidia wakulima wa maeneo ambayo wamefika katika kuwapa elimu ya VICOBA, hapa wakulima kwa kuongozwa na maafisa Maendeleo ya jamii huanzisha Vikundi vya kuweka na kukopa fedha na kupewa elimu ya utunzaji wa fedha hivyo ikiwemo kufungua akaunti za benki.

Lengo kubwa hapa ni kuwawezesha wakulima waweze kujinunulia vifaa vya kutengeneza uzio wa pilipili( Uhifadhi wa Tembo)