Suleiman Abeid,TimesMajira Online, Shinyanga
MRADI wa ujenzi wa reli ya kisasa(SGR) kutoka Isaka hadi Mwanza unatajwa kubadili hali ya uchumi wa wakazi wa Kata ya Sekebugoro wilayani Kishapu mkoani Shinyanga na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.
Hali hiyo imebainishwa na wakazi wa Kata ya Sekebugoro kwenye mahojiano maalumu na waandishi wa habari ambao wametembelea kata hiyo, kuangalia utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli hiyo katika maeneo hayo.

Durushi Maige na Macklina Wilbert wamesema uchumi wa wakazi wa Kata ya Sekebugoro kwa sasa ni mzuri na vijana wengi wamepata ajira katika mradi huo wa ujenzi wa reli ya kisasa na baadhi yao wameweza kujenga nyumba kwa ajili ya makazi yao.
“Kabla ya huu mradi hali yetu ya kiuchumi haikuwa nzuri, wengi wetu tulikuwa tunategemea kilimo ambacho kwa kiasi fulani ili uweze kupata mavuno mazuri itategemea hali ya masika ilivyo, mvua zikiwa za kutosha tunapata mazao ya kutosha lakini zikiwa haba ni majanga.Kupitia mradi huu wapo waliopata ajira wengine wanatoa huduma kwa wafanyakazi wanaotekeleza mradi mfano mamalishe, kiujumla hali zetu zimeboreka,” ameeleza Macklina.
“Baada ya kuanza kwa mradi wa SGR manufaa ni mengi yameonekana, baadhi ya wananchi wakazi wa kijiji hiki wamenufaika, vijana wamepata ajira na wameweza kujikwamua kiuchumi, wamejenga nyumba, wamenunua mifugo, mimi binafsi nimefungua kibanda cha biashara, mambo ni mazuri, ” ameeleza Khalid Abdalah Mkazi wa kijiji cha Seke Ididi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Sekebugoro,Mala Mathias,amesema ujio wa mradi wa ujenzi wa reli hiyo katika kijiji chake umewezesha kubadili hali za kimaisha kwa wakazi wengi ambao wamejenga nyumba za kisasa na kufanya muonekano wa kijiji kupendeza tofauti na miaka ya nyuma.

Ferdinand Mpogomi Diwani wa Kata ya Sekebugoro, amesema anaamini mradi huo wa kisasa ambao ni wa kimkakati utabidilisha mazingira ya kitanzania na kuwezesha usafiri wa kisasa na haraka ikilinganishwa na treni ya zamani pamoja na kupandisha thamani ya mazao ya wakulima katika maeneo yake.
Kwani watasafirisha mazao kwa urahisi kupeleka kwenye masoko makubwa ambako watapata bei nzuri tofauti na hivi sasa ambapo wanunuzi wa mazao yao wengi ni walanguzi wanaotoa bei ndogo.
Meneja Mradi wa kipande cha Isaka mkoani Shinyanga hadi mkoani Mwanza, Mhandisi Christopher Kalist,amesema mpaka sasa mradi huo umeweza kutoa ajira kwa watu zaidi ya 13,000 na wanaendelea kuajiri kulingana na mahitaji yanapojitokeza.
Amesema katika mradi huo kuna kazi za aina mbalimbali ikiwemo za kitaalamu na zile ambazo mtu yeyote anaweza akafanya na kipaumbele ni wakazi wa maeneo husika na wapo wataalamu ambao huchanganywa na wasio na ujuzi ili waweze kuwaelekeza kazi inavyofanywa.

Pia amesema,walianza kwa kujenga tuta ambalo limefikia asilimia 80, na sasa wapo wanaojenga stesheni huku matarajio ya kukamilika kwa mradi huo ni mwaka 2026 iwapo mambo yatafanyika kama yalivyopangwa,hivyo ametoa wito kwa Watanzania hasa wale ambao wanaishi kandokando ya reli hiyo kuwa walinzi wa miundombinu ili isiweze kuhujumiwa.
“Kiuchumi maeneo mengi ambayo mradi huu umepita kipato cha wananchi kimeboreka, mfano mzuri ni kwa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambayo tayari imepima viwanja vya makazi na biashara katika eneo la Kata ya Sekebugoro eneo ambalo mradi ulipoanza palikuwa kama porini, sasa thamani ya ardhi hapa imebadilika,” ameeleza.


More Stories
Mpogolo ajiandikisha kwenye daftari la Mpiga kura
TIB yawekeza bil.630.3 kwenye miradi ukiwemo wa kupunguza njaa
Kampeni ya UEFA Priceless: Chanja Kijanja, Shinda na Ufurahie Fainali za UEFA na Mastercard ya Benki ya Exim