Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Kwimba
Wakazi 24,349 wa vijiji vya Hungumalwa,Buyogo,Ilula na Kibitilwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza,kuondokana na changamoto ya maji kupitia mradi wa maji Hungumalwa ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 95.
Mradi huo ulianza kutekelezwa Machi 8,2022 na unatarajia kukamilika Agosti 15,2024 kwa
mkataba wa zaidi ya bilioni 10.5 kupitia Mkandarasi Emirate Builders Company Limited na kusimamiwa na wataalamu wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA).
Ambapo chanzo cha maji katika mradi huo ni Ziwa Victoria kutoka bomba kuu la KASHWASA linalopita Kijiji cha Mhalo na unatekelezwa kupitia fedha za GoT.
Hayo yamebainishwa Julai 27,2024 na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kwimba Godliver Gwambasa,wakati akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew aliyetembelea na kukagua utekelezaji wa mradi huo.
Gwambasa ameeleza kuwa lengo la mradi huo ni kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Hungumalwa kutoka asilimia 59 mpaka kufikia asilimia 100.
“Wananchi wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama,ambapo tumepanga kuwaunganishia wateja 500 maji nyumbani na
mpaka sasa wateja 466 sawa na asilimia 93 tumewaunganishia huduma ya maji,”.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Hungumalwa walioanza kupata huduma ya maji kupitia mradi huo akiwemo Mama Nangale ameeleza kuwa kabla ya mradi hali ilikuwa mbaya.
“Tulikuwa tunatoka nyumbani kufuata maji mbali pia tulikuwa na mabwawa ambayo hayana maji safi na salama, tunamshukuru sasa tunapata maji safi na salama,”.
Loveness Kuzenza Mkazi wa Mwambaya Kata ya Hungumalwa,awali tulikuwa wanaamka usiku kupanga foleni kwa ajili ya kufuata maji huku wakitumia saa saba ili kuyapata.
“Katika kupanga foleni watu walikuwa wanafanya ugomvi,watu wanasukumana na kusukuma ndio kama hauna nguvu huyapati maji kwa haraka,sasa tunapata maji kwa urahisi na karibu,naimani mradi ukikamilika kwa asilimia 100, kila kaya itapata maji kila siku,”.
Naye Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew,amesema kama Wizara kazi yao ni kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maji kwani jicho la Rais lipo katika sekta hiyo ili ikamilike kwa wakati na ubora unaohitajika kwani fedha nyingi zimetolewa.
Mhandisi Kundo amesema mtandao wa maji katika eneo hilo unazidi kuimarisha ili wananchi wapate maji safi na salama na kuhakikisha Watanzania waondokane na magonjwa yanayosababisha na matumizi ya maji yasiyo salama.
Pia ameielekeza MWAUWASA pamoja na RUWASA,kuhakikisha inabaini maeneo ambayo wanazalisha maji mengi safi,wategemee kutakuwa na maji taka mengi yatakayokuwa yanazalishwa na wakiaacha yakazagaa watarajie kutakuwa na changamoto ya magonjwa hivyo ni vyema wakajipanga sasa kuweka miji salama kwa kujenga miundombinu itakavyokuwa inaondosha maji taka.
“Idadi ya watu hapa Hungumalwa ni takribani 24,000,ukiwapa maji safi ya kutosha tutegemee kuna maji taka ya kutosha yatazalishwa,tukiyaacha vilevile maana yake tutakuwa tumewaokoa kutumia maji machafu ya kwenye mabwawa lakini bado tukawarejesha kwenye maji taka,wakati umefika wataalamu kuhakikisha tunatoka kwenye maboksi na kuanza kufikiria mbali,kuona namna gani tunaanza kuchukua hatua kabla ya jambo halijatokea kwa kufanya hivyo nchi itakuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama, mazingira salama zaidi kutokana na uwepo wa miundombinu ya kuondoa maji taka,”.
Sanjari na hayo Mhandisi Kundo amesema mahitaji mpaka sasa kwa Jiji la Mwanza ni lita za maji milioni 188 kwa siku huku uzalishaji ukiwa ni lita milioni 138 hivyo kuna upungufu wa lita milioni 50.
“Mradi wa Usagara unaoanza kujengwa utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita za maji milioni 144 hivyo utakidhi mahitaji ya Jiji la Mwanza,”.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba