Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),Mkoa wa Mwanza imeridhishwa na ukamilishwaji wa mradi wa chanzo cha maji wa Butimba na ufanisi wake.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza,Michael Masanja ‘Smart’amedhihirisha hayo ,baada ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Nyamagana.
“Tumekuja kuangalia maendeleo ya mradi huu wa maji wenye manufaa na tija kwa wananchi wa Jiji na pembezoni,tumefarijika kuona umekamilika ni mzuri na unatoa maji,kwa niaba ya kamati tunawapoongeza na tumeridhika nao,” amesema Smart na kuongeza;
“Maelekezo ya CCM kwa MWAUWASA hakikisheni mnaharakisha mpango wa usambazaji maji mradi ulete matokeo yanayokusudiwa na kuwanufaisha wananchi sambamba na kuusimamia kwa karibu uwe endelevu.”
Aidha amempongeza Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA Neli Msuya kwa kazi ya usimamizi na kuagiza utunzwe uwe endelevu na kuelekeza wananchi wasambaziwe huduma ya maji vinginevyo mradi hautakuwa na maana.
Naye Mwenyekiti kwa CCM Wilaya ya Nyamagana, Peter Bega, amesema maji ni kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Jiji la Mwanza,chanzo hicho kitakuwa chachu ya ushindi wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.
Amesema chanzo cha Butimba kukamilika kwake kutakisaidia chanzo Capripoint kuzalisha maji na hivyo wanazo sababu za kuwaeleza wananchi za kuichagua CCM kutokana na kutekeleza miradi ya kimkakati kwa weledi mkubwa.
Amesema CCM itafanya kila linalowezekana wananchi wapate maji ukizingatia amfanya kazi kubwa ya kukiheshimisha Chama na MWAUWASA kwa wananchi.
Awali akitoa taarifa ya mradi kwa Kamati,Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA,Neli Msuya amesema pamoja na kukamilika kwa mradi wa Butimba na kutoa huduma ya maji,hatua inayofuatia ni ya kuboresha mfumo wa usambazaji maji kwa kuongeza mtandao wa bomba na kujenga matanki makubwa ya kuhifadhia maji.
Ameainisha maeneo yatakayojengwa matanki hayo kuwa ni Buhongwa na Fumagila ya ujazo wa lita milioni 10 kila moja, Nyamazobe na Kisesa kila moja lita milioni 5 na Usagara milioni 1.
“Kazi kubwa iliyobaki baada ya mradi kukamilika kwa asilimia 100 ni kusambaza maji kwa wananchi kupitia vituo viwili cha kutoka katika chanzo na kingine cha Sahwa, hivyo tunamshukuru Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa Sekta ya Maji kipaumbele cha kipekee,” amesema
Neli amesema awamu ya pili ya mradi ni kufanya uzalishaji wa maji katika chanzo cha Butimba kwa kutumia nguvu ya umemejua ambapo kwa sasa Butimba inazalisha lita milioni 48 huku Capripoint kikizalisha lita milioni 90 kwa siku na kufanya jumla ya lita milioni 138.
Kwa mujibu wa Neli,mradi wa Maji Butimba ulianza kutekelezwa Februari 2021 na ulikamilika Oktoba 31,2023,unatarajiwa kukabidhiwa rasmi kwa MWAUWASA Oktoba mwaka huu,ulio chini ya uangalizi wa mkandarasi SOGEA SATOM.
More Stories
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake