Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
UTEKELEZAJI Mradi wa Kufua Umeme kwa maji wa Julius Nyerere unaendelea kushika kasi,ambapo baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa kuzindua uchepushwaji wa maji kwenye handaki ili kupisha ujenzi wa tuta kuu la bwawa la Nyerere.
Ujenzi wa tuta kuu umeshaanza kwa upande wa kushoto wa mto Rufiji na hivi sasa umefikia hatua ya uwekaji wa mabomba mawili kati ya matano ambayo yatatumika kupeleka maji kwenye vijiji vinavyopata maji kupitia mto Rufiki pamoja na matumizi ya viumbe hai.
Akielezea mabomba hayo,Mhandisi Kamgenyi Luteganya ambaye ni Mtaalamu wa bwawa kutoka kwa Mkandarasi Mshauri (TECU),amesema maji yakisha pita kwenye mabomba yanaendelea kwenye mkondo wake wa mto kama kawaida.
“Mabomba haya yanatosheleza mahitaji ya wananchi pamoja na viumbe hai vilivyopo kwani yatakuwa yanapitisha mita za ujazo 200 kwa sekunde” amesema Mhandisi Luteganya.
Ameongeza, ikifikia hatua ya kuanza kujaza bwawa ambapo inatarajiwa Novemba mwakani, handaki mchepusho litazibwa kwa mageti maalumu, ili kutoathiri shughuli za kibinadamu zinaendelea maji yatapitishwa kupitia mabomba hayo.
Kwa upande wake Mhandisi Dismas Mbote ambaye ni Mtaalamu wa Ujenzi Njia za Maji kutoka TANESCO, amesema ujenzi wa tuta unaendelea na kwa eneo la katikati ambalo maji yalikuwa yakipita zinajengwa kingo zuizi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ujenzi wa tuta kuu sehemu ya katikati.
“Upande wa kulia wa mto tumekamilisha hatua ya uchimbaji na hivi sasa tunaendelea na zoezi la uwekaji wa zege” amesema Mhandisi Mbote.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba