Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online
IMEELEZWA kuwa magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) ikiwemo minyoo na kichocho bado ni tatizo hasa maeneo ya Kanda ya Ziwa.
Ambapo watu bilioni 2 duniani wameathirika na minyoo ya tumbo,zaidi ya watu milioni 300 wameathirika sana huku watu 155,000 kila mwaka duniani hufariki kutokana na magonjwa hayo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinakadiria takribani asilimia 52 ya Watanzania sawa na watu milioni 22 wana maambukizi ya ugonjwa wa kichocho na minyoo ya tumbo.
Huku tafiti zikionesha na kuendelea kuonesha nchini hapa maeneo ya Kanda ya Ziwa ikiwa na maambukizi ya asilimia 50 hadi 80 au 90 ya magonjwa hayo yaliyokuwa hayapewi kipaumbele.
Akiwasilisha mada katika kikao cha uraghibishi na uhamasishaji kilichofanyika mkoani Mwanza hivi karibuni,Mhadhiri wa Chuo Kikuu Katoliki cha Sayansi na Tiba za Afya Bugando(CUHAS), Profesa Huphrey Mazigo,anasema magonjwa 17 kikiwemo kichocho na minyoo yaliyo Ukanda wa Tropiki yanaikumba jamii masikini vijijini zinazoishi chini ya Dola 2 na zisizo na uwezo wa kugharamia tiba na athari kwa watoto wa umri wa kwenda shule.
Prf.Mazigo anasema,kichocho ni ugonjwa unaosababishwa na minyoo aina ya schistosoma inayoishi kwenye mwili wa binadamu katika mishipa midogo ya damu.
Anaeleza kuwa ugonjwa wa kichocho huathiri mamilioni ya watu duniani na kwa kiwango kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa huo yapo barani Afrika ambapo Tanzania ni moja ya nchi zilizo athirika na ugonjwa huo ambapo maeneo yaliyoathirika sana ni Ukanda wa Ziwa Victoria na Pwani ya Bahari ya Hindi.
Anasema,jamii zinazoishi kando kando ya ziwa,mto na zinazo jishughulisha na kazi ya uvuvi na ukulima wa mpunga kwenye majaruba huathiriwa kwa kiwango kikubwa na ugonjwa wa kichocho ambao huathiri sana watoto wenye umri wa kwenda shule,wanawake na wanaume.
Anasema,takwimu za Shirika la Afya Duniani zinakadiria takribani asilimia 52 ya Watanzania sawa na watu milioni 22 wanaishi na ugonjwa wa kichocho.
Huku anasema ugonjwa wa minyoo hujulikana kama minyoo ya tumbo huathiri zaidi jamii masikini ambapo kuna aina tatu ya minyoo ambayo husababisha ugonjwa huo ikiwemo mnyoo mviringo,mnyoo mjeledi na mnyoo wa safura.
Pia anasema,ugonjwa huo uambukizwa kwa kula mayai ya minyoo hiyo kutoka katika udongo au kwa minyoo hiyo kupenya kwenye ngozi.
“Tanzania ni moja ya nchi zilizoathiriwa na ugonjwa wa kichocho hasa bonde la Ziwa Victoria hususani wakulima, wavuvi na watoto ambapo watu bilioni 2 duniani wameathirika na minyoo ya tumbo,zaidi ya watu milioni 300 wameathirika sana huku 155,000 kila mwaka duniani hufariki kutokana na magonjwa hayo,”anasema.
Mratibu wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) Mkoa wa Mwanza, Dkt.Mabai Leonard,anasema ugonjwa wa kichocho na minyoo ya tumbo bado ni tatizo kubwa Kanda ya Ziwa hususani Mkoa Mwanza.
Dkt.Mabai anasema takribani Watanzania milioni 22 wanaugua kichocho na minyoo ya tumbo huku tafiti zimeonesha na zinaendelea kuonesha kwa maeneo ya Kanda ya Ziwa maambukizi ya kichocho ni asilimia 50 mpaka 80 au 90.
Kwa maana unapoongelea kati ya watu 10, watu 5,7 au 8 wanakichocho halikadhalika na minyoo,hivyo uwepo wa kichocho bado ni tatizo kubwa katika Mkoa wa Mwanza kutokana na jiografia yake ya kuwa na maji mengi, shughuli za kilimo (majaruba ya mpunga) asili ya madimbwi ya maji hivyo wananchi wako kwenye hatari ya kupata magonjwa hayo.
Anasema,sababu ya magonjwa hayo kutokupewa kipaumbele ni kutokana na kutokuwa na dalili za haraka ambazo zinamfanya mtu achelewe kwenda kutafuta huduma ya matibabu tofauti na magonjwa mengine ambapo mtu anapata homa kali au kutapika haraka haraka anakimbia hospitali.
Pia anasema,ugonjwa wa kichocho unambukizwa na minyoo ya kichocho ambayo inabebwa na konokono ambao uishi kwenye maji kwaio mtu akiwa anafanya shughuli zake au makazi katika maeneo ya maji kwa vyovyote vile anaweza kupata ugonjwa wa kichocho.
Ili konokono aweze kubeba mayai hayo lazima mwanadamu awe na mayai ya kichocho na kuyatoa aidha kwa njia ya haja kubwa au mkojo.
“Endapo mtu atajisaidia katika vyanzo vya maji na akatoa yale mayai moja kwa moja yatakwenda kubebwa na wale konokono ambapo kule wataweza kumea na kuzaliana na kuwa katika hali ya kuwa mnyoo unaoweza kuingia kwenye mwili wa binadamu hivyo kuleta madhara ya ugonjwa wa kichocho,” anasema Dkt.Mabai.
Anaeleza kuwa kuna aina mbili za ugonjwa wa kichocho ambao ni kichocho cha tumbo na kichocho cha kibofu cha mkojo na kwa Kanda ya Ziwa tafiti zimeonesha ugonjwa wa kichocho cha tumbo umekua na nafasi zaidi kuliko kichocho cha kibofu cha mkojo.
“Vichocho vyote viwili vipo kwenye maeneo yetu lakin kichocho cha tumbo kipo kwa asilimia kubwa na hiki kinaleta madhara kwenye tumbo katika mfumo wa damu ambao inaweza kusababisha ini likapata shida au bandama likapata shida,na mwisho wa siku mishipa ya damu itakuwa imeathirika au mtu anaweza akatapika damu na akapoteza maisha.Mbali na kutapika damu anaweza akatoa damu katika sehemu ya haja kubwa kwaio mishipa ya damu inakuwa imeharibiwa,”anasema Dkt.Mabai.
Hata hivyo anasema,kichocho cha kibofu cha mkojo kinaenda kuathiri mfumo wa mkojo hivyo unakuwa umeathiri kibofu cha mkojo ambapo muathirika wa ugonjwa huo anaweza kuwa anakojoa damu hivyo kuweza kupata madhara makubwa ya kupata kansa ya kibofu cha mkojo
Kwa hiyo tunaona ni vyema jamii ifahamu kuwa tatizo lipo na wajumuike katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
Pia anasema,mtu anaweza kuishi na mayai ya ugonjwa wa kichocho au minyoo kwa miaka mingi bila ya mtu mwenyewe kufahamu lakini ataanza kupata dalili pale madhara yameisha kuwa makubwa.
Ambapo dalili moja wapo ni kichefuchefu,kutapika, kuwashwa, kukojoa damu,kutapika damu ingawa unaweza ukatapika damu ikawa siyo kichocho wakati mwingine ni vidonda vya tumbo.
“Mtu anaweza kuwa na kichocho asiwe na dalili na anapoanza kuonesha dalili tayari ameisha pata madhara makubwa mtu anapoanza kutapika damu au kansa ni madhara makubwa tayari,” anasema.
Hata hivyo anasema,ili kukabiliana na tatizo hilo Mkoa wa Mwanza umeandaa kampeni ya utoaji wa dawa za kingatiba kwa watoto wa umri wa miaka 5 hadi miaka 14 wa shule za msingi zote ambapo milioni 288.474(288,474,400) zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo.
Katika kufanikisha zoezi hilo anahimiza Halmashauri zote mkoani Mwanza zihakikishe watoto watakaopewa dawa kinga wapate chakula saa mbili kabla ya kumeza dawa hizo aina ya Albendazole kwa ajili ya minyoo ya tumbo na Prazequantel ya kichocho na wapewe kulingana na urefu wao.
“Kama nilivyosema watu wote wapo katika hatari ya kupata maambukizi lakini tunavyotoa dawa hizi ,lengo ni kuhakikisha kwamba katika kudhibiti na kutibu ugonjwa wa kichocho kuna mbinu mbalimbali ndio maana tunasema ujenzi wa vyoo na kunawa mikono hiyo ni njia moja wapo,dawa za kinga tiba pia.
“Lakini kuna yale makundi ambayo ni hatari zaidi ikiwemo watoto wadogo,pia tumekuwa na miradi mbalimbali kwa Wilaya ya Nyamagana na Ilemela ikiwemo mradi wa udhibiti endelevu wa kichocho na kampeni ya ugawaji wa dawa kwa watu wazima katika sehemu zote,”anasema Dkt.Mabai na kiongeza
“Hivi karibuni kuna mradi wa udhibiti wa kichocho ambao ukielekeza pia nguvu zake katika Wilaya ya Ukerewe ambayo ni Kisiwa na ina visiwa vingi sana kwa hiyo hizo juhudi za kuhakikisha kwamba watu wote tunawafikia ipo na ndio mpango wa Serikali na wadau na kwa kuanza tunahakikisha watoto tunawakinga na ugonjwa wa kichocho kwa sababu wao ni taifa la kesho,”
Kadhalika anasema,ili kudhibiti magonjwa hayo katika Mkoa wa Mwanza, Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya mapambano ya ugonjwa wa kichocho pamoja na kuwa na juhudi jumuishi za kuhakikisha vyoo vinajengwa katika mialo.
Kwa upande wake Kaimu Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, Oscar Kaitaba,anasema magonjwa hayo yanasababisha madhara kwa binadamu ikiwemo ulemavu wa muda mrefu, kuathiri maendeleo na makuzi ya watoto,kupunguza uwezo wa utendaji na hivyo kusababisha umasikini kwenye jamii.
Kuharibika kwa mimba,unyanyapaa hasa kwa wasichana na wanawake,utapia mlo kwa watoto,upungufu wa damu mwilini ,udhaifu ambao unaweza kukaribisha magonjwa mengine,presha ya ini,kansa ya kibofu cha mkojo,upofu,utoro shuleni na uwezo duni wa kuelewa masomo pamoja na kuacha shule.
Kwa upande wake mmoja wa wakazi wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Judith Mkatesi, anasema ipo haja ya Serikali kupitia Wizara ya Afya kuhakikisha inatoa elimu kila wakati juu ya magonjwa ya kichocho na minyoo.
Pia anasema sema,waende mbali zaidi kwa kutembelea na kuelimisha watu wanaoishi kando kando ya ziwa na kufanya shughuli zao ziwani.
Anasema, pia wawahimize watu wanaoishi kando ya ziwa kujenga vyoo bora na kuzingatia matumizi sahihi ili waache kukidhi haja zao vichakani na pembeni mwa ziwa huku serikali ikihakikisha inaboresha mazingira yao na kuwapatia huduma muhimu.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika