November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa ‘FUM’ kuboresha huduma za afya, maji Tabora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MRADI wa Marafiki wa Urambo na Mwanhala (Friends of Urambo and Mwanhala-FUM) unaotekelezwa katika Wilaya za Urambo na Kaliua Mkoani hapa unatarajiwa kuongeza upatikanaji huduma za afya na maji katika vijiji mbalimbali Mkoani hapa.

Mradi huo unaofadhiliwa na marafiki kutoka nchini Uingereza unatarajiwa kutekelezwa katika vijiji zaidi ya 9 vilivyoko katika Wilaya hizo na utahusisha uchimbaji visima virefu, ujenzi wa zahanati na wodi ya mama na mtoto.

Mratibu wa Mradi huo Lucky Enock, ameeleza hayo juzi alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili aliyetembelea na kujionea mradi wa maji na wodi ya mama na mtoto iliyojengwa katika Kijiji cha Kiloleni Wilayani Urambo.

Alisema utekelezaji mradi huo ulianza Mei 20, 2022 ambapo walianza na ujenzi wa mradi wa maji ya bomba kwa kuchimba kisima kirefu na kujenga wodi ya mama na mtoto (RCH) katika zahanati ya Kijiji cha Kiloleni kata ya Kiloleni.

Alibainisha kuwa wodi hiyo imekamilika na kuanza kutumika na mradi wa maji umefikia asilimia 98 ambapo kiasi cha sh mil 42.4 kimetumika, kazi iliyobaki ni kukamilisha ufungaji wa mfumo wa malipo kabla ya kutumia (pre paid), maji tayari yanatoka na wananchi wameanza kuyatumia.  

Enock alifafanua kuwa Taasisi hiyo imeamua kujikita katika utekelezaji miradi hiyo ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alitaja maeneo ya kipaumbele yatakayonufaika na huduma hiyo ya maji safi ya bomba kuwa ni kwenye zahanati, shule za msingi, sekondari, eneo la soko, makanisa, misikiti na kwenye makazi ya wananchi.

Alibainisha baadhi ya vijiji vitakavyonufaika na miradi hiyo katika wilaya hizo kuwa ni Kiloleni, Usisya na Kamalendi (Ukondamoyo) katika Wilaya ya Urambo na Usimba, Maboha, Nyasa, Uhindi na Ibambo katika Wilaya ya Kaliua.

Mbunge wa Jimbo la Urambo Magreth Sitta alipongeza taasisi hiyo na kubainisha kuwa miradi hiyo imekuja wakati mwafaka ili kusaidia juhudi za serikali za  kupunguza kero ya upatikanaji huduma za afya na maji katika maeneo mengi.

Aliongeza kuwa kutekelezwa kwa miradi hiyo kutasaidia sana kuboreshwa huduma za afya na kuongeza upatikanaji huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa vijijini hususani katika wilaya hizo na nyingine.