Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Utekelezaji wa mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba umefikia asilimia 96 huku ukitarajiwa kufanyiwa majaribio Septemba 15, mwaka huu ambao kukamilika kwake kutasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa maji jijini Mwanza.
Mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba unatekelezwa kwa gharama ya bilioni 69, utazalisha kiasi cha lita za maji milioni 48 kwa siku na utahudumia zaidi ya wakazi 450,000.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 12,2023 na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Neli Msuya,wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi na Kamati ya Usalama Wilaya Nyamagana kwenye mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba akiwa ameambatana na Menejimenti ya MWAUWASA.
Neli amesema utekelezaji wa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 96 huku majaribio ya mradi yatakayoanza Septemba 15,2023 ni hatua ya awali kuelekea katika hatua ya ukamilishwaji.
Ambapo wanakwenda kwa awamu, majaribio hayo yatawapa matokeo chanya katika upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi ambao wataanza kuona mabadiliko kadri siku zinavyokwenda.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi amesema utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa maji Butimba unakwenda vizuri na kasi inaridhisha.
Makilagi ameeleza kuwa ziara hiyo imelenga kujionea maendeleo ya mradi kuelekea siku ya majaribio ya awali ya mradi huo Septemba 15, 2023 huku akiipongeza MWAUWASA kwa kasi hiyo ya utekelezaji wanayoendelea nayo.
“Niipongeze pia timu iliyoundwa na Jumaa Aweso, Waziri wa Maji kwa ushirikiano huu mnaoutoa kwa MWAUWASA, tuna imani tutapata matokeo chanya,” amesema Makilagi.
More Stories
Rais Dkt.Samia asajili timu ndani na nje ya Nchi kukabili Marburg
RUWASA Katavi yasaini mkataba ujenzi bwawa la Nsekwa
Wapanda miti 500,kumbukizi ya kuzaliwa Dkt.Samia