Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza
Mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba umefanyiwa majaribio ya awali ya mitambo ili kuanza kutoa huduma ya maji kwa wakazi 450,000 kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo Sawa,Kishiri,Kisesa watakaonufaika na mradi huo.
Mradi huo ulioanza kutekelezwa Februari Mosi,2021 kwa gharama ya bilioni 70,umefikia asilimia 96 huku ukitegemewa kukamilika na kukabidhiwa Oktoba 31,2023 na kidogo kidogo wananchi wataanza kuona matunda ya mradi.
Akitoa taarifa ya mradi huo Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza(MWAUWASA) Neli Msuya,mara baada ya kufanyika kwa majaribio ya awali yaliofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza CPA.Amosi Makala kwa kuwasha pampu moja kati ya tano za kusukuma maji safi katika chanzo hicho cha maji Butimba ameeleza majaribio hayo ni kiashiria kuwa mradi unaenda kukamilika.
“Tumeanza majaribio ya kuwasha pampu za mitambo yetu ya chanzo hiki kipya cha maji za kusukuma maji kwenda kwenye maeneo yetu ya kituo cha kusukuma maji cha Sawa ambacho kitasukuma maji kwenda kwenye tenki la Igoma,”ameeleza Msuya.
Msuya ameeleza kuwa kwa mujibu wa makadirio mahitaji ya Jiji la Mwanza na vitongoji vyake ni lita za maji milioni 165 kwa siku ambapo chanzo pekee cha maji kilichokuwepo cha Capripoint kinauwezo wa kuzalisha kiasi cha lita milioni 90 za maji kwa siku.
Hali hiyo iliosababisha kuwa na upungufu wa lita milioni 75 za maji kwa siku na kuilazimu MWAUWASA kutoa huduma ya maji kwa mgao hasa katika maeneo ya miinuko ambayo ni mengi kwa mji huu na yalio pembezoni mwa Jiji.
Ameeleza kuwa kufuatilia upungufu huo serikali ilianza kutekeleza mradi wa chanzo kipya cha maji Butimba wenye thamani ya jumla ya bilioni 70 ambapo mkataba huo ulisainiwa Juni 2020,kati ya MWAUWASA na kampuni ya Sogea Satom.
Pia ameeleza kuwa mradi huo ambao utazalisha lita milioni 48 za maji kwa siku utaboresha huduma ya upatikanaji wa maji safi kwa Jiji la Mwanza huku maeneo yatakayonufaika moja kwa moja ni pamoja na Nyegezi,Mkolani, Buhongwa, Lhahima, Fumagila, Sawa, Igoma,Kishiri, Nyamh’ongolo na Kisesa huku maji ambayo yalikuwa yameelekezwa katika maeneo haya toka chanzo cha Capripoint sasa yatapelekwa katika maeneo mengine.
“Majaribio ya mradi huu ambao umewasha yana ashiria kukamilika kwa mradi na kuongeza thamani katika maeneo hayo, tunawakumbusha wananchi wa maeneo hayo kuwa tupo katika majaribio hivyo katika kipindi hiki wachemshe maji ya kunywa,” ameeleza Msuya na kuongeza kuwa
“Tukipiga hesabu hapa zile lita milioni 90 na hizi lita milioni 48 itakuwa jumla ni lita milioni 138 huku mahitaji ni lita milioni 165, bado tutakuwa na upungufu wa lita mlioini 27 hivyo tunakwenda kuongeza uzalishaji wa maji chanzo cha Capripoint kwa lita milioni 54 ambapo wiki ijayo tutatangaza zabuni ya kutafuta Mkandarasi hivyo kuongeza uwezo kutoka kuzalisha lita milioni 90 za maji hadi lita milioni 144,”.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makala ameeleza kuwa suala la maji ni agenda kwa Jiji hilo hivyo mradi wa Butimba kutoa maji ni heshima kwa CCM na wananchi ambao wakiulizwa wanataka nini kati ya maji na Katiba mpya watasema maji.
Makala ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo ni pigo na habari mbaya kwa wapinzani wa serikali waliotarajia mradi kutokamilika na kwenda kuutumia katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu kama fimbo ya kuitandika CCM.
“Maji ni kilio cha muda mrefu,Rais Samia amekisikia na kukitatua kwa vitendo,jukumu lililobaki viongozi mkawaelimishe wananchi,wawaeleze yaliyofanywa na serikali pia mabomba yaliyopokelewa yasifikishwe kimya kimya,pia wananchi chukueni tahadharu msinywe maji bila kuchemsha mradi bado upo kwenye majaribio wapo wenye fitina watasena ni machafu,”.
Mwenyekiti wa Bodi ya MWAUWASA, Christopher Gachuma amesema serikali imetumia fedha nyingi kujenga mradi huo na majaribio hayo ni ishara unaelekea kukamilika,hivyo wananchi waitunze miundombinu hiyo na zikipatikana bilioni 60 za vyanzo vingine zitamaliza tatizo la maji Mwanza.
Naye mmoja wa wananchi wa Jiji la Mwanza waliohudhuria hafla ya majaribio hayo Kabula Barnabas ameeleza kuwa maji yalikuwa yanawasumbua na mradi huu umekuwa kama nuru kwa wananchi wa Mwanza hivyo wananchi wenzake watunze miundombinu ya maji pia wazingatie matumizi mazuri ya maji ili yawanufaishe wengi.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu