October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa boost wapunguza msongamano wa wanafunzi

Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Mwanza

UONGOZI wa shule mpya ya msingi Shilabela,wilayani Misungwi, umeipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuboresha sekta ya elimu ikiwemo kujenga miundombinu ya madarasa na matundu ya vyoo na kununua samani.

Pongezi hio imetolewa leo na Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo, Modester Aloyce baada ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mwanza,kukagua ujenzi wa shule hiyo msingi Shilabela uliogharimu sh. milioni 540.3 kupitia mradi ya BOOST ukiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025.


Amesema shule hiyo yenye wanafunzi 1,035 imejengwa na serikali mwaka 2022/23 ili kupunguza msongamano wa watoto katika shule ya msingi Mbela yenye wanafunzi 2,610 huku mundombinu ikiwa haikidhi mahitaji.

“Serikali imeboresha sekta ya elimu ya msingi kwa kuleta fedha za kujenga jengo la utawala la shule ya Shilabela,ofisi 4 za walimu,madarasa 16,matundu 27 ya vyoo vya wanafunzi wa awali,msingi na walimu,”amesema.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza,Michael Masanja ‘Smart’ kwa niaba ya Kamati ya siasa baada ya kukagua mradi huo wa BOOST amesema,serikali imeboresha elimu husasani ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa samani.

Samrt amekiri kuwa madarasa hayo ya mradi wa BOOST yamejengwa kwa kiwango cha ubora huku akitoa rai kwa wanafunzi kusoma kwa bidii wafaulu kwa kiwango cha juu ili kuifanya shule hiyo iwe ya mfano pia waitunze miundombinu hiyo idumu kwa kizazi cha sasa na vijavyo.

Awali kamati hiyo ilikagua na kuridhishwa na mradi wa mabweni mawili ya wasichana Misungwi Sekondari yaliyogharimu milioni 192

“Niwapongeze kwa usimamizi mzuri wa fedha za miradi hii ya mabweni ya wasichana,rai yangu someni kwa bidii na kufaulu kwa daraja la kwanza,ukosefu wa umeme hilo litashughilikiwa watoto wasome hata usiku,”amesema Smart na kuahidi kuwapelekea Luninga wapate taarifa na kufahamu yanayofanywa na serikali yao.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Shule hiyo, Alnold Rwiza bweni moja limekamilika kwa milioni 62 litachukua wanafunzi 94 na jingine linalojengwa kwa milioni 129 wanatarajia kuchukua wanafunzi 194, lengo ni kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia,changamoto ni kutounganishwa na nishati ya umeme.