Na Mwandishi Wetu,Timesmajira online Mwanza
SERIKALI imesema,utekelezaji wa Mradi wa BOOST unatarajiwa kuboresha kiwango cha elimu na fursa za upatikanaji wa elimu kwa watoto wa elimu ya awali na msingi Tanzania Bara huku malengo mahsusi ya mradi huo yakiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu, kuinua ubora wa walimu wa shule za awali na msingi na usimamizi na utawala bora katika utoaji huduma ya elimu.
Akizungumza jijini Mwanza wakati wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mradi huo, Mratibu wa Mradi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Lawrence Mselenga amesema ufuatiliaji huo unafanyika kuona hali halisi ya utekelezaji wa afua mbalimbali katika ngazi ya Halmashauri.
Ametaja afua hizo kuwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kwa elimu ya awali na msingi na kwamba katika utekelezaji wake awamu ya kwanza yatajengwa madarasa yasiyopungua elfu tatu, ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule zilizopo ikiwa ni pamoja na kujenga shule mpya katika maeneo yasiyokuwa na shule hali inayosababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Afua nyingine ni pamoja kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu kufuatia utekelezaji wa mpango wa shule salama ikiwa ni pamoja na kuongeza uandikishaji kwa watoto wa elimu ya awali katika asasi za elimu nchini.
Mselenga ametaja afua nyingine ambayo ni kuboresha uwezo na umahiri wa walimu katika ufundishaji na ujifunzaji darasani pamoja na maudhui kwa walimu, kuimarisha walimu kwa kuendeleza mafunzo ya walimu kazini, kugharimia utoaji wa elimu, kuboresha mwalimu katika matumizi ya TEHAMA kwenye ufundishaji, kuboresha mazingira ya shule kupitia Halmashauri zinazokidhi vigezo vya usimamizi na utawala bora wa elimu.
“Tunakwenda kuangalia namna Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ngazi ya Mkoa, Halmashauri, Kata, Mitaa, vijiji, vitongoji na shule zilivyojipanga kutekeleza afua hizi zote, kubaini changamoto na kisha wataalamu wetu kwa kushirikiana na wale wa kutoka benki ya Dunia kutoa ushauri na namna ya kuweka mipango stahiki ya kufanikisha utekelezaji wa afua za mradi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika mradi wa BOOST,” alisema Mratibu Mselenga
Ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa BOOST umefanyika katika Mikoa mitatu ambayo ni Lindi, Dar es Salaam na Mwanza.
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari