March 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi ujenzi matenki matano ya maji wafikia asilimia 15

*Kamati ya Bunge uwekezaji wa mitaji ya umma yataka mradi ukamilike kwa wakati 

*Wakazi 450,000 kunufaika na mradi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa matenki matano ya maji yenye ujazo wa lita  milioni 31, umefika asilimia 15,ambayo yanajengwa katika  maeneo Kisesa,Buhongwa,Usagara, Fumagila na Nyamazobe.

Huku Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma(PIC),imeiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA), kuhakikisha  mradi wa huo  unakamilika kwa wakati ili kutatua changamoto ya hupatikanaji wa maji kwa wananchi.

 Hayo yameelezwa Machi 21,2025  na Mwenyekiti wa PIC Vuma Augustine, wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kutembelea  mradi wa ujenzi wa matenki matano ya maji na kituo  cha kusukuma maji eneo la Sahwa,wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.

Vuma amesema, baada ya Serikali kujenga chanzo cha maji Butimba, sasa inafanya kazi ya kusambaza maji kwa wananchi ndio maana imeanza utekelezaji wa ujenzi wa matenki hayo ili maji yaweze kuwafikia.

“Tunaamini mradi huu utaenda kuwa suluhisho la hupatikanaji wa maji jijini Mwanza,na dhamira ya kumtua ndoo mama kichwani itakuwa imefanikiwa.Rai yetu MWAUWASA itaendelea kumsimamia Mkandarasi ili tupate mradi bora na ukamilike kwa wakati ili tija yake ifanyike na miundombinu italindwa kwa matumizi ya leo na kesho,”amesema Vuma.

Kaimu Mkurugenzi wa MWAUWASA Neli Msuya, amesema kutokana  na changamoto ya maji,walilazimika kuandaa mradi maalumu wa kuboresha usambazaji wa maji ambao ni ujenzi wa matenki matano.

Matenki hayo  yatakua  ujazo wa lita milioni 31 kwa gharama za bilioni 46.2, kwa ufadhili wa Serikali  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa.Ambapo mkataba ulisainiwa Juni 13,2024 na utekelezaji wake ulianza rasmi Desemba 24,2024 na utakamilika Desemba 24,2026, na Mkandarasi amelipwa  kianzio  bilioni 8.6.

Neli amesema,mradi huo utahusisha ujenzi wa vituo viwili vya kusukuma maji na mabomba makuu ya kusafirisha maji,kutoka katika vituo vya kusukuma maji kwenda kwenye matenki,ambao  kwa kiasi kikubwa unatekelezwa  Wilaya ya Nyamagana na kiasi  kidogo Magu na Misungwi.

“Wakazi 450,000,watanufaika baada ya mradi kukamilika ni wa maeneo  ya Buhongwa, Nyamazobe,Nyahingi,Luchelele,Lh’wahima,Sahwa,Fumagila,Kishiri na Igoma kwa Wilaya ya Nyamagana,Wilaya ya Magu ni  Bujora,Kisesa na Kanyama  huku Wilaya Misungwi ni  Usagara,”amesema Neli.

Kwa upande wake Meneja Miradi wa MWAUWASA, Celestine Mahubi,amesema tenki la maji linalojengwa Sahwa katika kituo cha usambazaji  maji litakuwa na uwezo wa kubeba maji lita milioni 3, ambalo litasambaza maji  kwenye matenki ya Kisesa Nyamazobe, Fumagila na Usagara.

“Nina  imani mradi huu utakamilika kwa wakati kwani utekelezaji kwa sasa upo asilimia 15 lakini muda  ambao Mkandarasi ametumia ni asilimia 12 ya muda uliopangwa na kabla ya kuanza mradi huo tuliwashirikisha wananchi,”amesema.

Mmoja wa wananchi wa Mtaa wa Sahwa,Mpemba Babugejeshi,amesema awali walikuwa wanafuata maji maeneo ya mito na walikuwa wanapata ahueni mvua zinaponyesha,lakini baada ya kuja kwa mradi huo wameanza kuota maji kwenye magati ingawa bado changamoto ya upatikanaji maji ipo katika maeneo hayo.

“Tunaimani  mradi unavyozidi kuendelea na ukikamilika utatusaidia kutatua changamoto ya maji,hivyo tunaomba ukamilike kwa wakati ingawa tenki la kwanza lilivyokamilika tulipata ahueni ya maji kupitia magati ingawa nayo hayatoshi,”.