December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi Mashindei umeongeza upatikanaji maji Korogwe

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

MRADI wa maji Mashindei na visima kumeongeza upatikanaji wa huduma ya maji hadi kufikia asilimia 88 kutoka asilimia 32 ya upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe mkoani Tanga.

Uzalisha umeongezeka wa lita za maji4,138,000 kwa siku hivyo kufanya uzalishaji wa sasa uwe jumla ya lita 5,523,000 kwa siku sawa na asilimia 88 ya mahitaji ya lita 6,289,000 kutoka asilimia 32 iliyokuwepo kabla ya kutekelezwa ujenzi wa miradi huo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga Francis Komba (kushoto) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Tito Mganwa (kulia) wakiwa kwenye Baraza la Madiwani.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) Mhandisi Yohana Mgaza kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Korogwe kwenye taarifa ya utekelezaji wa shughuli ya mamlaka hiyo kwa kipindi cha Aprili hadi Juni, 2023.

Mhandisi Mgaza ameeleza kuwa miundombinu ya utoaji wa huduma ya maji inajumuisha vyanzo, matanki 15 yenye jumla ya lita za ujazo 3,100 na mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilomita 156 ambapo mamlaka ya Maji Korogwe ina maunganisho ya wateja wapatao 5,379 na wote wamefungiwa dira za maji na upotevu wa maji ni wastani wa asilimia 39.

Madiwani wakiwa kwenye Baraza la Halmashauri ya Mji Korogwe.

“Kutekeleza uchimbaji wa visima saba katika maeneo ya Majengo, Kwasemangube, Mbeza mawe, Manzese, Mtonga, Mgambo na Kwakombo, ambapo ujenzi wake umekamilika huku mradi wa maji Mashindei ambao hadi hivi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 90,kukamilisha ujenzi wa nyumba za pump tatu za Majengo, Manzese na Kwakombo,kulaza mabomba kutoka kwenye visima na kufunga pampu za kusukuma maji kwenda kwenye matenki ya kuhifadhia maji Manzese, Kwasemangube, Majengo na Mbeza Mawe,”.

Mhandisi wa HTM Bahati Ngowi akizungumza kwenye Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Korogwe.

Pia ameeleza kuwa ukusanyaji wa madhuli yatokanayo na mauzo ya maji na maunganisho mapya ambapo kwa mwezi April – Juni, 2023, namlaka ilikusanya zaidi ya milioni 77 huku ilipokea fedha kutoka Mfuko wa Maji wa Taifa kwa ajili ya uchimbaji wa visima, ununuzi wa pampu na kufunga pump za Mbeza Mawe, Kwasemangube, Manzese, Mtonga, Majengo na Kwakombo na ununuzi wa mabomba kwa ajili ya mradi wa Maji Mashindei na kufanya manunuzi ya Fittings.

Mhandisi Mgaza amesema changamoto iliyopo kwenye Mji wa Korogwe ni uchakavu wa miundombinu iliyojengwa siku nyingi ambayo haijawahi kufanyiwa ukarabati wowote hasa mabomba ya usambazaji maji katika maeneo ya katikati ya mji huo ikiwemo Mtonga, Masuguru, Manundu Kati, Mbeza, Majengo, Kwamkole, Old Korogwe na Manzese.

Pia kupasuka kwa mabomba katika maeneo ambayo yalikaa muda mrefu bila kuwa na maji, ukosefu wa miundombinu ya kusafisha na kuchuja maji (Water Treatment Plant), hivyo kufanya maji yanayozalishwa kutokuwa na ubora hasa nyakati za mvua.

“Katika kukabiliana na changamoto zilizopo hapo juu mipango ifuatayo inahitaji kutekelezwa ambayo ya muda mfupi ni kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji Mashindei kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maji,kukamilisha ufungaji wa pampu ya maji katika kisima cha Kwakombo, kuboresha miundombinu ya kusambaza maji kwa kulaza bomba lenye urefu wa kilomita 24.9 katika Mji wa Korogwe.

“Mipango ya muda mrefu ni ujenzi wa mradi wa maji kwa kutumia chanzo cha mto Ndemaha, ambapo litajengwa dakio, kulaza bomba urefu wa kilomita 21, kutekeleza ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye uwezo wa kujaza lita 2,000,000 eneo la Kwamkole, kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya kusafisha, kuchuja na kutibu maji (Water Treatment Plant) kwa ajili ya kuhakikisha maji yanawafikia wananchi yakiwa safi na salama tofauti na ilivyo hivi sasa,” amesema Mhandisi Mgaza.

Wakuu wa Idara na Vitengo wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Korongwe

Mhandisi Mgaza amesema pia, utekelezaji wa mradi wa Miji 28, ambapo Mji wa Korogwe ni moja ya miji itakayonufaika na mradi huo hadi sasa mkandarasi yuko eneo la mradi anaendelea na ukusanyaji wa vifaa vya utekelezaji (Site Mobilization), ambapo mabomba kwa ajili ya utekelezaji wa mradi yameanza kuwasili kwa ajili kazi.

Mgaza amesema, kutokana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Halmashauri ya Mji Korogwe ilikuwa na watu wapatao 86,551 kati yao 70,971 sawa na asilimia 82 ya wakazi wote katika Mji wa Korogwe wanapata huduma ya maji kwa mgao.

Vilevile amesema, mamlaka inahudumia wakazi wa Korogwe kutoka kwenye vyanzo vya maji vya Mto Mdogo wa Mbeza, Mto Mashindei, Mto Pangani (eneo la Mtonga na Old Korogwe), na visima virefu sita vilivyopo maeneo ya Majengo, Kwasemangube, Mbeza mawe, Manzese, Kwameta na Kwakombo. Vile vile katika chanzo cha HTM kwa wakazi wa kata ya Mgombezi.

Mamlaka ya Maji HTM ambayo imekabidhiwa jukumu la kuhudumia Mji wa Korogwe, inahudumia eneo lote la kiutawala la Halmashauri ya Mji Korogwe lenye jumla ya kata 11, mitaa 22 na vijiji 7.

Kwa sasa Mamlaka inatoa huduma ya Maji kwenye maeneo hayo kwa kutumia vyanzo mbalimbali isipokuwa Kijiji kimoja tu (Mahenge) ambacho kwa sasa kuna mradi wa maji unaoendelea kujengwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).