Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar
MKUU wa wilaya ilala, Edward Mpogolo ameitaka jamii ya watanzania kuendelea kuwalinda na kuthamini mchango wa wazee katika taifa.
Mpogolo ameyasema hayo leo Oktoba Mosi 2024, wilayani Ilala alipozungumza na mwandishi wa mtandao huu kuhusu siku ya wazee dunia inayoadhimishwa Oktoba Mosi kila mwaka duniani.
Amesema katika siku hiyo muhimu jamii haina budi kutambua mchango wa wazee wote katika taifa, mikoa na wilaya kwani wao ndiyo wahasisi wa amani, umoja na mshikamano katika taifa ikiwa pamoja na kushiriki kwenye maendeleo.
Amesisitiza kuwalinda na kuwatunza wazee ni jukumu la jamii, hasa familia kuhakikisha wazee wanaendelea kuwa na mchango wa mawazo ili kupata hekima, busara na mawazo yao.
Aidha,amekemea tabia ya kuwadharau wazee na kuwatenga katika familia kwani umri wao unahitaji uvumilivu na kuwaweka karibu kuliko kuwapeleka katika kufanya kazi ngumu wakati ndugu bado wapo.
Akizungumzia suala la maadili na malezi kwa jamii ya sasa amesema, wazazi wawarithishe watoto tabia njema za kuwaheshimu wazee na kuwapisha katika vyombo vya usafiri vya umma ambapo iko changamoto kubwa ya malezi kuwapisha wazee katika siti.
“Wazee ni tunu katika Taifa letu, hivyo inapaswa tuwaheshimu na kuwalinda lakini pia wao ndiyo waasisi wa amani katika nchi yetu, lakini pia nitoe wito kwa watu wote hususani vijana kuonesha heshima kwa wazee wetu kwa kuwasaidia pale wanapohitaji msaada na hususani katika vyombo vya usafiri pindi unapoona Mzee ameingia na hakuna sehemu ya kukaa kumpisha kwani mbali na heshima pia unapata baraka”,amesema Mpogolo
Amesema wilaya ya ilala itaendelea kuwasikiliza na kuwasaidia wazee wenye chamgamoto ili wapate huduma kwa wakati katika ofisi za umma.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua