May 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpogolo akabidhi Cheti kwa wahitimu

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

KAMPUNI ya Serengeti Breweries Limited (SBL), kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), wamefanya mahafali ya kwanza ya programu ya mafunzo ya ukarimu kwa vijana chini ya mpango wa SBL wa “Learning for Life”, wenye lengo la kuwajengea vijana wa Kitanzania ujuzi wa vitendo katika sekta ya ukarimu na utalii.

Mahafali haya, yaliyofanyika katika kampasi ya NCT jijini Dar es Salaam, yalikutanisha wanafunzi 109 waliohitimu, wadau wa sekta ya ukarimu, pamoja na viongozi wa serikali, huku Mgeni rasmi wa hafla hiyo akiwa, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo na Mgeni Maalum akiwa Dkt. Pindi Chana (Mb), Waziri wa Maliasili na Utalii.

Imeelezwa kuwa, mpango huo ulioanza Septemba mwaka jana ni sehemu ya mkakati mpana wa SBL wa Society 2030, Spirit of Progress, ukilenga kuwawezesha vijana kupitia mafunzo ya vitendo, masomo darasani na mafunzo kwa vitendo kazini ili wawe tayari kuajiriwa kwenye soko la ajira linalokua la utalii na ukarimu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Pindi alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa kupitia utalii shirikishi:

“Utalii siyo tu kusafiri ni injini ya ukuaji wa uchumi jumuishi, ajira kwa vijana na kubadilishana tamaduni. Tanzania inalenga kufikia watalii milioni 5 kwa mwaka na programu kama hizi zinahakikisha tunajenga rasilimali watu sahihi kufanikisha lengo hilo “, alisema Waziri Pindi.

Alibainisha kuwa Serikali imeanzisha vifurushi vipya vya vivutio vya utalii, vikiwemo utalii wa chakula, ili kutangaza utajiri wa vyakula vya asili vya Tanzania.

“Watalii wa leo wanatafuta uzoefu wa kweli, Sasa tunawaletea vyakula vya asili vya Kitanzania ‘vyakula vya asili’ – kama sehemu ya vivutio vya utalii. Kutoka kwenye chakula safi, kisicho na kemikali moja kwa moja kutoka shambani, hadi vyakula vya kipekee vya mikoa mbalimbali, utalii wa chakula utawawezesha watalii kujifunza utamaduni wetu huku pia tukikuza uchumi wa jamii zetu,” alisema Waziri.

Aidha, alisisitiza kuwa utalii ni lazima uwe endelevu, shirikishi, na wenye manufaa kwa jamii, huku akipongeza ushirikiano kati ya SBL na NCT “Ushirikiano huu ni mfano wa ubunifu ambapo vijana wanapewa ujuzi siyo tu wa ajira, bali wa kujenga taaluma endelevu zinazoweka mbele maadili, utamaduni na huduma bora kwa watalii wetu.

Aidha kwa upande wake, Edward Mpogolo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, aliipongeza programu hiyo kwa kuchangia katika jitihada za Serikali kukuza sekta ya utalii “Sekta ya utalii na ukarimu nchini Tanzania ina fursa kubwa ya kuzalisha ajira na kuchochea maendeleo ya taifa.

“Programu kama hii siyo tu kwamba inawapatia vijana wetu ujuzi, bali pia inasaidia kutekeleza dira ya Serikali ya kugeuza utalii kuwa nguzo ya maendeleo jumuishi na endelevu. Nawapongeza SBL na NCT kwa dhamira yao ya kuwawezesha vijana wa Kitanzania kwa vitendo”, alisema Mpogolo.

Programu hiyo iliwafundisha wanafunzi ujuzi katika mawasiliano, uongozi, uwasilishaji binafsi, usimamizi wa muda, upangaji wa bajeti na huduma kwa wateja. Kupitia Diageo Bar Academy, walipata pia mafunzo maalum ya uendeshaji wa baa, huduma kwa wateja, na sanaa ya mchanganyiko wa vinywaji (mixology), Ili kuhakikisha uendelevu.

Imeelezwa kuwa, SBL ilianzisha pia programu ya kuwajengea uwezo wakufunzi wa NCT (Training of Trainers – ToT), ili waweze kufundisha programu hiyo kwa kujitegemea kwa awamu zijazo.

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Dkt. obinna Anyelebechi alisema, “Mahafali haya siyo tu kusherehekea mafanikio ya kitaaluma, bali ni wakati wa mabadiliko. Tunajivunia sana wanafunzi hawa na tunashukuru kwa ushirikiano wa NCT. Kupitia ‘Learning for Life’, tunafungua milango ya ajira na kuwawezesha vijana kufanikisha ndoto zao katika sekta ya utalii na ukarimu inayokua kwa kasi hapa Tanzania”, alisema.

Nae Dkt. Florian Mtey, Mkuu wa NCT, alisifu mpango huo alisema “Programu hiyo imefungua milango kwa wanafunzi, inawapeleka nje ya darasa na kuwapa uzoefu halisi wa kazi, kuwajengea kujiamini na kuwafanya kuwa tayari kwa soko la ajira la leo. Tunajivunia ushirikiano huu na tunatazamia kuupanua zaidi.

Mahafali haya ni ushuhuda wa mafanikio yanayopatikana kupitia ushirikiano wa kimkakati kati ya sekta ya umma na binafsi, na ni sehemu ya dhamira ya SBL katika kuendeleza jamii kupitia programu jumuishi na endelevu. Programu ya Learning for Life itaendelea kufikia vijana zaidi na kuimarisha msingi wa sekta ya ukarimu kote nchini. Alisema.