March 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpogolo ajiandikisha kwenye daftari la Mpiga kura

Na Heri Shaaban, Timesmajira Online,Ilala

MKUU wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo Machi 20,2025, ameshiriki zoezi la kujiandikisha katika maboresho ya Daftari la Mpiga Kura mtaa wa Karume Kata ya Ilala.Zoezi ambalo limeanza Machi 17 hadi 23,2025.

Mpogolo alifika Mtaa wa Karume saa tatu asubuhi ambapo alipanga foleni pamoja na mwananchi kisha kujiandikisha katika daftari hilo.

“Wananchi wa Wilaya ya Ilala tujitokeze kujiandikisha katika Daftari la Mpiga Kura, Mkoa Dar es Salaam tumepewa wiki moja tuwe wote tumejiandikisha,ili tuje kumpigia kura Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, Wabunge na Madiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025,”alisema Mpogolo

Amesema ili uweze kupata haki yako ya kupiga kura, kila mmoja lazima awe amejiandisha kwa kufuata taratibu eneo analoishi.

Hivyo amewataka Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Wajumbe,kushirikiana kuhamasisha wananchi kujiandikisha katika vituo vyao.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Karume,Hajji Bechina,amesema katika eneo la mtaa wake zoezi linaenda vizuri ambapo siku ya ufunguzi mpaka leo watu wanajitokeza kujiandikisha.