Na Mbaraka Kambona,TimesMajira online, Dodoma
SERIKALI imezindua mpango wa unywaji maziwa kwa Watumishi wa Umma kwa lengo la kuhamasisha unywaji wa maziwa yanayozalishwa ndani ya nchi lakini pia kuongeza kipato cha wafugaji.
Akizindua mpango huo jijini Dodoma jana, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema kuwa utekelezwaji wa mpango huo utasaidia kutatua changamoto ya soko la maziwa na kuleta tija kwa wafugaji.
Waziri Ndaki amesema kuwa lita za maziwa zinazozalishwa na wafugaji nchini ni bilioni 3 lakini maziwa yanayochakatwa kwa mwaka ni milioni 74.3 na hivyo kufanya maziwa mengi kupotea kwa kukosa soko la uhakika jambo ambalo sio zuri kwa mustakabali wa tasnia ya maziwa.
” eo tunazindua awamu ya kwanza ya unywaji wa maziwa kwenye Ofisi za Serikali na kwa awamu hii ya kwanza tumeanza na wizara kumi, lakini kutakuwa na awamu nyingine ya uzinduzi zitakazohusisha wizara, taasisi na mashirika ya umma,” amesema Ndaki
Amesema kuwa uzinduzi huo unakwenda sambamba na ugawaji wa majokofu ya kutunzia maziwa kwa wizara hizo huku akitumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi katika wizara,watumishi na wananchi kwa ujumla kuunga mkono mpango huo.
Ameongeza kuwa unywaji wa maziwa katika ofisi za umma utainua kwa kiwango kikubwa soko la maziwa yanayozalishwa nchini na kuepuka unywaji wa maziwa kutoka nje ya nchi, na hivyo kukuza pato la wafugaji pia itachochea upatikanaji wa ajira.
Ndaki amesema itakua ni jambo la ajabu kuona Ofisi ya Serikali inaagiza maziwa yanayotengenezwa kutoka nje wakati Serikali imezindua mpango mahususi unaohamasisha unywaji wa maziwa yanayozalishwa nchini.
Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini, Dkt.George Msalya amesema ana imani kuwa kama ofisi zote za Serikali ambapo watumishi wa umma wanafika takribani Laki Tano zitaunga mkono unywaji huo wa maziwa itakua ni fursa nzuri na pana ya kukuza soko la maziwa ya ndani.
Wizara ambazo zimehusishwa katika awamu hiyo ya kwanza ya uzinduzi wa unywaji wa maziwa unaoratibiwa na Bodi ya Maziwa ni pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda na Biashara, TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Elimu.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi