*Serikali kuchangia nusu bei gharama za chanjo
*Vijana,wanawake kupata ajira
*Wafugaji,wataalam wahimizwa ushirikiano.
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi,itaanza mpango wa utoaji wa chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa kuanzia Januari 2025.
Ambapo bilioni 28.1,zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mpango huo, unaolenga kudhibiti na kutokomeza magonjwa ya mifugo nchini.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni ya chanjo za mifugo kitaifa uliofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete,Desemba 18, 2024 jijini Dodoma, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Ashatu Kijaji, amesema mpango huo utakaotekelezwa kwa miaka mitano kutoka 2024-2029.
Utagharimu kiasi cha bilioni 216 zitakazotolewa na Serikali,ambapo bilioni 28.1 zitatumika awamu ya kwanza ya uchanjaji na utambuzi wa mifugo kuanzia Januari 2025.
“Mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga bilioni 28.1, kuchanja mifugo dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu ya ng’ombe,ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na ugonjwa wa mdondo wa kuku ili kuwasaidia wafugaji wetu kote nchini,” amesema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji amesema, awamu ya kwanza ya mpango huo wa chanjo Serikali kupitia wataalamu wa sekta ya mifugo na Mamlaka za Serikali za Mitaa, itachanja ng’ombe zaidi ya milioni 19.0,dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu ya ngo’mbe (CBPP).
Mbuzi na kondoo milioni 20.9, dhidi ya ugonjwa wa sotoka ya mbuzi na kondoo (PPR) na Kuku wa asili milioni 40,dhidi ya ugonjwa wa mdondo wa kuku (ND),lengo la Serikali ni kutoa chanjo kwa mifugo angalau asilimia 70 ya idadi ya mifugo husika kwa miaka mitano mfululizo.
“Kwa sasa hali ya uchanjaji kwa ng’ombe, mbuzi na kondoo ni asilimia 21,kuku wa kienyeji asilimia 40 na kuku wa kisasa ni asilimia 100.Kampeni hii itasaidia kutokomeza magonjwa ya mifugo, kutoa ajira za muda mfupi kwa vijana na wanawake 3540 na kuongeza usafirishaji wa nyama nje ya nchi kutoka asilimia 14 ya sasa na kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2029,”amesema Dkt.Kijaji.
Dkt. Kijaji amesema katika kufanikisha zoezi la chanjo ya mifugo,Serikali itachangia nusu bei ya gharama za chanjo ili kuwarahisishia wafugaji kuchanja mifugo yao.
“Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,ameahidi kuwa Serikali itachangia nusu ya bei kwa ajili ya chanjo kwa mifugo ambapo kwa upande wa ng’ombe itachangia shilingi 500, kwa upande wa mbuzi na kondoo itachangia shilingi 300 na upande wa kuku itakchangia shilingi 100,”Dkt. Kijaji.
Hivyo akuwataka viongozi wa mamlaka ya serikali za mitaa, manispaa na majiji kutoa ushirikiano kwenye kampeni hiyo ya chanjo na kisha kueleza umuhimu wa chanjo za mifugo kwa taifa na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema zoezi hilo la chanjo litahusisha wataalam na wafugaji .
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Taifa (CCWT),Mrida Mshota,amesema zoezi la chanjo linalokuja kwa awamu hii litawasaidia wafugaji hasa kukabiliana na magonjwa ya mifugo.Hivyo aliiomba Wizara kuupa kipaumbele pia ugonjwa wa miguu na midomo (FMD).
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais