December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpango wa kilimo wa uwezeshaji wanawake kiuchumi kuleta tija nchini

Na Grace Semfuko, MAELEZO

NCHINI Tanzania kumekuwepo na jitihada za muda mrefu za kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia kwenye maeneo mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, jitihada hizo kwa kiasi kikubwa zimeonesha mabadiliko ya kisera, sheria na hata taratibu mbalimbali kuhakikisha zinazingatia haki na usawa wa kijinsia.

Ajenda ya usawa wa kijinsia imekuwa ikitoa msisitizo kuhusu nafasi ya wanawake katika maendeleo. Tafiti, sera na miongozo mbalimbali imekuwa ikisisitiza kuwa mwanamke ni kiungo muhimu katika safari ya kuyafikia maendeleo ya kweli katika jamii zetu na katika nchi yetu huku mkazo mkubwa ukiwa ni ushiriki wa wanawake katika maendeleo.

Sekta ya kilimo kwa ujumla inaelezwa kuchangia zaidi ya robo ya pato la taifa (takribani asilimia 30), huku ikitoa fursa ya ajira kwa mamilioni ya watu, ambapo inaelezwa kuwa sekta hiyo kuwa ndio muajiri mkuu nchini. Nazo tafiti zinaonesha, wakati asilimia 64 ya wanaume wote huelezwa kujihusisha na kilimo, idadi ya wanawake ni kubwa zaidi, ambapo takribani asilimia 70 ya wanawake wote nchini wanajihusisha na kilimo.

Wakati Tanzania ikizalisha kwa wingi na kujitosheleza kwa chakula, ni dhahiri pasipo shaka kuwa kuna mchango mkubwa sana wa wanawake hasa wa vijijini katika kuyafikia matokeo hayo.

Hali hiyo ya nafasi muhimu ya wanawake katika kilimo inadhihirika pia kote Barani Afrika ambapo tafiti zinaonyesha kuwa wanawake wanazalisha asilimia 60 hadi 70 ya chakula chote kinachozalishwa katika ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara.

Sababu hiyo inaifanya Dunia kutambua nafasi kuu na adhimu ya wanawake kama wazalishaji wa msingi vijijini.

Pamoja na kuwa na mchango mkubwa katika uzalishaji, wanawake pia wanahudumu katika nafasi nyingine kadhaa na za muhimu katika sekta nzima ya kilimo. Miongoni mwa nafasi hizo, wanawake wanahudumu kama chanzo cha uzalishaji, usambazaji na urithishaji wa maarifa na ndio wanaotunza jamii, suala ambalo si muda wote jamii inaliona kama muhimu.

Kutokana na mchango mkubwa wa kilimo, kiuchumi na kijamii barani Afrika na nchini Tanzania hususani katika sekta ya kilimo, wadau mbalimbali wamevutika wafanyabiashara, wanasiasa, wasomi.

Nao wadau hao kwa kutambua nafasi kubwa na kuu waliyonayo wanawake katika kilimo, wameamua kujihusisha na wanawake katika kile wanachokieleza kuwa ni mchango katika maendeleo ya kilimo na ukombozi wa wanawake katika kilimo.

Mpango wa kilimo wa kuwawezesha Wanawake kiuchumi ni mpango ambao upo katika mchakato wa majadiliano baina ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Kilimo pamoja na wadau wa mashirika ya maendeleo ya ndani ya nchi na ya kimataifa ambapo wadau wamekutana Jijini Dar es Salaam kujadili namna ya utekelezaji wa mpango huo.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dkt. John Jingu anasema Wizara hiyo kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ya jamii wa ndani na nje ya Nchi wameanza mkakati wa kutekeleza Mpango wa Kilimo wa uwezeshaji wanawake kiuchumi.

Mpango huo unakuja kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alilolitoa April 22 Bungeni Jijini Dodoma la kutaka Serikali yake kuweka nguvu katika kuwawezesha wanawake kiuchumi na kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Akizungumza katika mkutano wa wadau hao wa maendeleo kuhusu programu ya kilimo ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, Dkt Jingu amesema Wanawake wakiwezeshwa kiuchumi wataepukana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuimarisha uchumi katika familia zao.

“Lengo kuu la mpango huu ni kuondokana na ukatili wa kijinsia dhidi ya Wanawake, ni njia ya kimkakati ya kupambana na ukatili huu, ukatili mwingi wa kijinsia unaotokea hapa kwetu Tanzania mfano ndoa za utotoni, ukeketaji, ajira za watoto na nyinginezo nyingi chanzo chake kikubwa ni umasikini na matatizo ya kiuchumi, kwa hiyo ukiwawezesha wanawake kiuchumi utakuwa umewapa uwezo wa kukabiliana na umasikini na ukatili” anasema Dkt.Jingu.

Ikiwa wanawake ndio wazalishaji wakuu, kundi hili la jamii limewekewa msisitizo mkubwa katika kuendeleza ajenda ya kilimo biashara na kilimo cha kisasa. Kuanzia kwenye nafsi binafsi na kwenye vikundi vyao vya kimaendeleo na hata katika ngazi za familia.

Kwa upande wake mwakilishi wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) Nchini Tanzania Bi.Stine Hnydelger amesema nchi hizo zitaendelea kuisaidia Tanzania katika kuepukana na ukatili wa kijinsia.

“Umoja wa Ulaya tunafurahishwa na mpango huu wa Tanzania, ni mpango mzuri, kwa muda mrefu tumekuwa tukifanya kazi ya kusaisiana na nchi mbalimbali katika kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatoweka, tunaahisi kusaidiana nanyi kwenye hili” anasema.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kilimo Tanzania Timothy Mmbaga ameiomba Serikali kuangalia kwa karibu na kusimamia mifuko ya uwezeshaji wa wanawake kiuchumi iliyopo kwenye Halmashauri za Wilaya nchini.

“Kuna mifuko iliyowekwa na Serikali ya uwezeshwaji wanawake na vijana kiuchumi, mifuko hii ipo kisheria, katika mkakati huu tunaomba hili suala liangaliwe vizuri” anasema.

Mkutano huo wa kujadili mpango wa kilimo wa uwezeshaji wanawake kiuchumi umewakutanisha wadau kutoka katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto, Wizaya ya Kilimo, Mashirika yasiyo ua kiserikali ya hapa nchini, mashirika ya maendeleo ya kimataifa likiwepo la USAID pamoja na nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU).