Na Mary Margwe, Timesmajira Online,Tarime
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Raymond Matinda, ametangaza kuanzisha mpango wa ujenzi wa nyumba ya Katibu wa jumuiya hiyo kwa kushirikiana na kamati tendaji ya wilaya hiyo.
Akizungumza mara baada ya kikao kilicholenga kujadili mpango huo, Matinda amesema,lengo kuu ni kuweka mazingira bora ya kazi kwa mtumishi wa jumuiya hiyo, sambamba na kutekeleza agizo la muda mrefu la chama kuhusu uboreshaji wa makazi kwa viongozi wake.

“Tulikaa kikao cha kamati tendaji na kujadili kwa kina suala la ujenzi wa nyumba ya Katibu wa Jumuiya. Hili ni jambo la msingi kwa utendaji wa mtumishi wetu. Tutalifanya kwa umakini ili kumuwezesha kuondokana na maisha ya kupanga,” amesema Matinda.
Pia ameeleza kuwa,hatua hiyo ni mwanzo wa mchakato mpana wa kuboresha miundombinu ya jumuiya hiyo wilayani humo, kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utendaji wa viongozi wake.
“Tumeweka msingi mzuri wa mwelekeo huu. Tutaendelea kushirikiana na wanajumuiya pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha tunaifikisha ndoto hii mahali stahiki,”amesisitiza Matinda.
Amewahimiza wanachama wa Jumuiya ya Wazazi wilayani Tarime kumpa ushirikiano wa dhati katika kutekeleza mipango ya maendeleo waliyojiwekea, akibainisha kuwa mshikamano na moyo wa kujitolea ni silaha muhimu ya mafanikio.
“Bila ushirikiano wenu, mimi peke yangu sitaweza kufanikisha haya. Hivyo tushirikiane bega kwa bega, tukamilishe hili kwa wakati na tuendelee na majukumu mengine mengi ya jumuiya yetu,”amesema.

Sanjari na hayo amesisitiza nidhamu, mshikamano na moyo wa kujitolea miongoni mwa wanajumuiya ndio msingi wa kuhakikisha mafanikio ya mpango huo yanafikiwa kwa manufaa ya jumuiya na chama kwa ujumla.

More Stories
Waandikishaji wapiga kura watakiwa kuzingatia weledi
CCM Songwe yatoa onyo kwa makada wanaojipitisha kabla ya kampeni
Serikali yasisitiza utamaduni wa kujikinga mahali pa kazi