November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Moto wateketeza vyumba viwili vya madarasa shule ya sekondari Iyela

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

WATU wasiofahamika wamechoma moto vyumba viwili vya madarasa na kuteketeza madaftari yote ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Iyela iliyopo mkoani Mbeya.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mbeya, Malumbo Mgata amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huku na kueleza kuwa chanzo moto huo bado hakijafahamika.

Ambapo amesema kwamba walipata taarifa ya kutokea tukio hilo majira ya saa 7.47 asubuhi katika shule ya sekondari Iyela mtaa wa Iyela.

“Tulipata taarifa za uwepo wa moto na tulifanikiwa kufika eneo la tukio na kukuta moto unawaka kwenye madarasa mawili ambayo yalikuwa yanatumika kuhifadhia vitu mbalimbali vya wanafunzi vilivyokuwa vinatumika kujisomea,”amesema Kamanda huyo wa Zimamoto.

Ameeleza kuwa madhara yaliyotokea ni madaftari ya wanafunzi na vitu vingine vya muhimu ambavyo walikuwa wakitumia kujisomea shuleni hapo chanzo cha moto huo bado hakijafahamika na uchunguzi zaidi unaendelea.

Aidha Mkuu huyo wa Zimamoto ametoa rai kwa wananchi kutoa taarifa pindi yanapotokea matukio ya moto kwa namba 114 sanjari na kuwa walinzi wa mali za serikali kwani inatoa fedha nyingi kuwekeza katika sekta ya elimu .

Mwalimu Stephano Kamendu amesema madarasa hayo yalikuwa yakitumika kuhifadhia vifaa vya wanafunzi na inasemekana kuwa kuna mtu anayedaiwa kuwasha moto huo na kutokomea kusikojulikana.

Devotha Charles amesema kuwa walipigiwa simu kuwa kuna tukio la moto na kukuta watoto wanaojisomea wamefika na kukuta chumba kimejaa moshi.

Ambapo watoto hao walitaka kuingia kwenye vyumba vilivyokuwa vinaungua kwa lengo la kuokoa madaftari ,magodoro lakini waliwazui wasiiingie hivyo walianza kuleta mchanga ili kuzima moto huo lakini hawakuweza kuokoa chochote kwani vitu vyote vilishaungua na moto .

Elia Mwakafulu amesema kuwa moto huo ulikuwa mkubwa walijitahidi kuokoa lakini vitu vyote viliungua vilivyokuwepo kwenye madarasa hayo na kushukuru kuwa hakuna mtoto aliyepata madhara.

Kabla ya ujio wa Mwalimu Stephano Kamendu baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali walikuwa wakitumia baadhi ya maeneo hayo yaliyotajwa kama Chimbo kufanya vitendo vya uhalifu ikiwemo uvutaji wa bangi na ubakaji vitendo ambavyo kwa sasa vimedhibitiwa.