December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Moto ambao chanzo hakijajulika umeunguza vyumba 3,stoo 1

Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza

Moto ambao chanzo chake hakijajulika umeunguza vyumba vitatu na stoo moja katika jengo la ghorofa moja lenye wafanyabiashara zaidi ya 20 katika mtaa wa Rwagasore jijini Mwanza

Ajali hiyo ya moto imetoka majira ya saa tano asubuhi Oktoba 30,2023 mwaka huu katika mtaa huo huku jitihada mbalimbali zilizofanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,Jeshi la Polisi na wananchi zikizaa matunda na kuweza kudhibiti moto huo usisambaze maeneo mengine pamoja na kuuzima.

Akizungumza namna walivyoweza kudhibiti moto huo Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza Camila Raban, ameeleza kuwa walipo pokea taarifa ya tukio la moto katika mtaa huo gari lilifika kwa wakati.

Ambapo vyumba vilivyoungua kimsingi ni vitatu huko moto ulipo anzia na stoo moja ndogo huku vitu vilivyokuwa vinaungua ni vyenye asili ya plastiki kwa maana ya maputo ya kuchezea watoto pamoja na chupa zilizotengenezwa na plastiki.

Ameeleza kuwa moto ulipotokea majengo yake yamepangana katika hali ya maghorofa na moto umeanzia vyumba vya juu na ulipo anzia ndioo ulipoishia kwani hawajaruhudu kusogea na kusambaa katika chumba chochote cha mbele kazi kubwa ilikuwa ni kuzuia moto usitoke katika chumba uliko anzia kuelekea katika nyumba nyingine.

“Ndio maana mlikuwa mnaona moto mkubwa kwani plastiki pia ni sehemu ya gesi hivyo inawaka kwa ukubwa sana kwa mantiki hiyo Askari wamefanikiwa kupambana na moto na kudhibiti na hatimaye moto ukazimika na hali ipo shwari,”ameeleza Raban.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa moto unapoanza taarifa inapaswa kutolewa mapema ili wakute moto bado haujahama kwani vyumba ambavyo vinatunza plastiki ni chini ya dakika tano moto unaweza kuwa umesamba na kwenda kwenye chumba kingine na gari lao la kwanza limefika eneo la tukio chini ya dakika tano.

“Tunachoomba barabarani wanaposikia ving’ora vya gari ya Zimamoto wapishe maana ni maisha ya watu na mali za watu zinapotea,wananchi waendelee kupisha njia kama walivyofanya leo na gari likafika kwa wakati na moto umedhibitiwa haujaenda kwingine na bado chanzo cha ajali ya moto huu hakijajulikana,”

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa ameeleza kuwa
katika tukio hilo la moto ambalo limekuja katika hali ya ghafla ni kwamba majira ya saa tano na nusu Jeshi hilo lilipokea taarifa kwamba kuna moto unawaka katika jengo ambalo lipo katika mtaa wa Karuta na Rwagasore.

Baada ya taarifa hizo aliwatuma Askari wao kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na usalama wa watu na mali zao katika mitaa hiyo jambo ambalo kwa bahati nzuri waliofanikiwa.

Ameeleza mara moja vyombo vyote viliweza kufika eneo la tukio na jitihada za pamoja za kuzima zikianza kufanyika katika tukio hilo moto uliendelea kuwaka ambapo katika taarifa ya awali ni kuwa moto huo umeanzia stoo ya mama mmoja ambaye amefahamika kwa jina moja la Mama Riziki.

“Huyu ana stoo hapa juu kwenye hilo jengo ambapo anauza vifaa vya urembo na vifaa vingine vya kuchezea watoto,kwaio alikuwa amehifadhi mali zake huko na ndiko moto ulipo anzia lakini kwenye floor ya chini kulikuwa na duka la Bwana mmoja anaitwa Lucas Ndegama ambaye ni mfanyabiashara ambaye ameweza kuokoa mali zake zote kwa maana floor ya chini haikuweza kupata moto,”

Sambamba na hilo maduka mengine ambayo yalikuwa yamezunguka ndani ya jengo hilo upande wa chini, chini ya usimamizi wa jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wameweza kutoa mali zao ambazo hazikuteketea na moto.

“Kimsingi mali zote zilizokuwa juu kwa kiasi kikubwa zimeungua tumejitahidi kumtafuta huyo mama alijulikana kwa jina la Mama Riziki anayemiliki stoo huko juu katika jengo hilo lililopata moto ambaye kwenye eneo la tukio haonekani lakini bado tunamfuatilia kwa kushirikiana na familia yake kuona amekwenda wapi pengine amepata mshtuko kutokana na jambo hili ambalo limetokea tunaendelea kumtafuta ili kuona usalama wake upoje,”.

Ambapo ameeleza kuwa mpaka sasa hakuna mtu yoyote alipoteza maisha au kujeruhiwa kutokana na moto huo huku kiasi kikubwa cha mali kuokolewa na jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi wamefanya kazi kubwa ya kuweza kuzima moto ili usiweze kusambaa katika majengo mengine yaliopoa katika eneo hilo kwani ya mnasongamano wa watu na majengo yapo karibu karibu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi,ametoa pole kwa wale walipata majanga hayo huku imani yao vyombo husika vitabainisha chanzo cha moto huo.

“Niwaelekeze vyombo vyote vya uchunguzi ikiwemo Jeshi la Polisi vifanye uchunguzi kwa haraka ili kubaini chanzo cha moto na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kujilinda na majanga ya moto yana potokea,”ameeleza Makilagi.

Mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo ameeleza kuwa jengo hilo lililopata moto linawafanyabiashara zaidi ya 20 huku akieleza kuwa jeshi la Zimamoto limefika kwa wakati wamejitahidi licha ya changamoto ndogo ndogo zilizojitokeza na moto umefanikiwa kuzimwa.

“Tulianza kuona moshi unatoka katika chumba kimoja ambacho ni stoo ya mmoja wa wafanyabiashara hapa,hivyo tukakimbia kwenda kuokoa mali zetu kilichoendele kingine hatujui,”