January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Morogoro yajipanga uzalishaji korosho

Na Dotto Mwaibale, TimesMajira Online, Morogoro

WAKULIMA wa zao la korosho mkoani hapa, wameahidi kufanya mageuzi makubwa ya kilimo cha zao hilo, baada ya kuhamasika na programu maalumu ya mafunzo ya nadharia na vitendo, yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI).

Taasisi hiyo kupitia kituo chake cha Naliendele kwa sasa kinaendesha mafunzo ya kilimo bora cha zao la korosho kwa wakulima na Maofisa Ugani wa halmashauri zilizoko Mikoa ya Kanda ya Kati, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kusini lengo likiwa kuongeza tija na kuinua kiwango cha uzalishaji wa zao hilo.

Wakizungumza juzi kwa nyakati tofauti wakati wa mafunzo hayo yanayofanyika Shule ya Msingi Mnjilili, mji mdogo wa Gairo mkoani hapa, wadau hao wamesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka.

“Mafunzo haya yamenisaidia na kunipa mwanga wa namna ya kuboresha shamba langu la ekari mbili kwa sasa nina matumaini makubwa ya kulima kitaalamu zao hili,” amesema mkulima wa korosho kutoka Dumila, Samwel Dede.

Mkulima mwingine, Elizabeth Senyangwa kutoka Gairo amesema, kabla ya kupata mafunzo hayo miongoni mwao walikuwa kwenye mtazamo wa kustawisha zao hilo kimazoea. Lakini kwa sasa nimejifunza mengi hasa kwenye eneo la udhibiti wa wadudu na magonjwa na namna bora ya kuandaa shamba lake.

Naye Ofisa Ugani, Elina Dastan kutoka Kilosa amesema, anaona fahari kwa Tanzania kupitia watafiti wake kuzidi kubuni teknolojia mpya kwa ustawi wa sekta ya kilimo nchini.

“Ugunduzi wa teknolojia za aina zote hizi za mbegu bora za korosho kutoka TARI ni fursa kubwa kwa wakulima na Watanzania kwa ujumla,” amesema Dastan.

Kutokana na hamasa iliyotawala wakati mafunzo yakiendelea, wadau hao wa zao la korosho walitaka kufahamu kwa kina ni aina ipi ya mbegu za korosho ambazo ni bora zaidi na zinazaa kwa wingi kama mkulima atahitaji kupata mavuno zaidi.

Lingine lililojitokeza kwenye majadiliano ni je mbegu za zao hilo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, zinachukua muda gani hadi kuanza kuvunwa korosho yake sanjari na umakini wa palizi yake.

Akijibu maswali hayo Mratibu wa zao hilo kitaifa, Dkt. Geradina Mzena amesema mbegu zote zilizogunduliwa na kufanyiwa utafiti na serikali kupitia taasisi hiyo, zina ubora na zinafaa kwa matumizi ya mkulima katika kupata tija inayostahili.

Huku Mtafiti kutoka Kituo cha TARI Naliendele Mtwara, Kasiga Ngiha akisema mbegu za korosho zinazozalishwa na kituo hicho huchukua kati ya miaka miwili mpaka mitatu, kabla ya kukomaa na korosho yake kuanza kuvunwa.

%%%%%%%%%%%%%%%%