March 3, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Morogoro waitikia zoezi la uboreshaji Daftari la kudumu

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesema kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wananchi kujitokeza katika vituo mbalimbali vya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, unaofanyika mkoani Morogoro na sehemu ya mkoa wa Tanga kwa siku saba kuanzia Machi mosi hadi 7, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Rufani, Jacobs Mwambegele ameyasema hayo jana, alipokua akishuhudia zoezi la uboreshaji wa Daftari wa Kudumu la Wapiga Kura lilivyokuwa linaendelea katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero.

“Nimekuja kushuhudia jinsi zoezi hili linavyoendelea, Saa 2:00 kamili vituo vimefunguliwa na nimefika katika Kituo cha Mafiga B ambako kituo kilifunguliwa Saa 2 asubuhi na wananchi wengi sana wamejitokeza katika kuboresha taarifa zao au kujiandikisha kuwa Wapiga Kura,” amesema Jaji Mwambegele.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaani Jacobs Mwambegele (kulia) akiangalia namna mwendesha kifaa cha Biyometriki (BVR) anavyochukua picha wakati alipotembelea kituo cha Mafiga B Manispaa ya Morogoro mkoani Morogoro kuangalia zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililoanza mkoani humo Machi mosi na litafikia ukomo Machi 07, 2025. (Picha na INEC).

Amesema, ametembelea vituo vingi na wananchi wamejitokeza kwa wingi kuboresha taarifa zao au kujiandikisha na alitoa wito kwa wakazi wa Manispaa ya Morogoro na Mvomero na mkoa mzima wa Morogoro kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo.

“Nawasihi wakazi wa Manispaa ya Morogoro na Mvomero kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha au kuboresha taarifa zao, nawasihi wafanye hivyo mapema iwezekanavyo kwani zoezi hili limaenza leo na litachukua muda wa siku 7 mpaka hapo tarehe 7,2025,” amesema Jaji Mwambegele.

Amesema, Wananchi wasisubiri mwisho ndio wakaja kujiandikisha bali wafanye hivyo mapema na wasubiri tu tarehe ya Uchaguzi Mwezi Oktoba ili wapige Kura kuwachagua viongozi wanaowataka.

Akizungumzia changamoto iliyobainika na kufanya watu kukaa muda mrefu vituoni, Jaji Mwambegele amesema wamebaini kuna watu wamesahau majina yao waliyoyatumia kujiandikisha hapo awali hivyo hutumia muda mrefu kutafuta katika mfumo.

“Kunachangamoto kidogo imejitokeza katika kuwatafuta wale waliokuja kuboresha taarifa zao, wengi inachukua muda kumpata kwa sababu amesahu majina yake, jina la kwanza analiweka la pili au saa nyingine anakosea ‘speling’ kwa mfano wewe kama unaitwa Zaituni inaandikwa na ‘i’ mwisho au bila ‘i’ sasa unapotamka jina ambalo linatofautiana na lilivyo katika data base yetu inachukua muda kukupata,” amesema.

Amewasihi wananchi wakumbuke majina yao kama ni Khadija inaanza na K wakumbuke namna hiyo au kama ni Hadija ina anza na H wakumbuke namna hiyo na kama ni Mohammed au Muhammed wakumbuke katika kutamka majina yako vizuri.

Kwa mujibu wa ratiba, kwa sasa Tume imeanza Uboreshaji wa Daftari wa Kudumu la Wapiga kura mzunguko wa 12 kati ya mizunguko 13 iliyopangwa na Tume kwa mkoa wa Morogoro na Halmashauri Nne za Bumbuli, Handeni, Mkinga na Pangani zilizopo mkoani Tanga limeanza leo Machi mosi na litafika tamati Machi 07, mwaka huu, ambapo litadumu kwa siku saba huku vituo vikifunguliwa Saa 2:00 asubuhi na kufungwa Saa 12:00 jioni.

Wananchi wakiwa wamejitokeza kwa Wingi katika moja ya vituo vya Kata ya Mafiga Manispaa ya Morogoro kwaajili ya kuajindikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo zoezi hilo linaendelea Mkoani Morogoro kuanzia Machi mosi hadi Machi 07,2025. (Picha na INEC)