November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella (kushoto) akizungumza na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo alipomtembelea ofisini kwake. (Picha na Judith Ferdinand).

Mongella: Changamoto zitatuliwe kabla ya uchaguzi

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

WASIMAMIZI wa uchaguzi nchini wametakiwa kuhakiki vituo na maeneo yao wanayoyasimamia mapema ili kubaini changamoto zilizopo na kuzitatua kabla ya siku ya uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alipokuwa akizungumza na Mjumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ambaye alikuwa Jijini Mwanza kwa ajili ya mafunzo ya siku tatu ya Wasimamizi wa Uchaguzi wa Mikoa ya Mwanza na Mara alipokwenda kumsalimia ofisini kwake Jijini Mwanza, .

Mongella amesema, Ofisi yake itashirikiana na wasimamizi wa uchaguzi kufanya ukaguzi wa maeneo ya vituo vya kupigia kura ili kuona changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na miundombinu ya kufika kwenye vituo na kuyatatua kabla ya siku ya kupiga Kura.

Amesema, changamoto kubwa iliyopo katika maeneo ya visiwani hasa katika jiji la Mwanza akitolea mfano kisiwa cha Ukerewe ambacho baadhi ya maeneo yake lazima kutumia boti na mitumbwi ili ufike, hivyo ni lazima ijulikane mapema hali ya usafiri utakaotumika kwa ajili ya kuhakikisha vifaa vinafika salama na kurudishwa ili kufanikisha uchaguzi.

“Elimu itolewe na watu wajitokeze kupiga kura, tuondoe dhana ambayo imejengeka kwa baadhi yetu kuwa fulani ameshashinda na kwamba kila kitu kipo sawa na kuacha kwenda kupiga kura, ni vema wananchi wakaelemishwa umuhimu wa kujitokeza kupiga kura,” ameasema Mongella.

Kwa upande wa Jaji Mstaafu Thomas Mihayo amesema, kuelekea uchaguzi mkuu ujao Tume imeshaanza kusambaza vifaa vya uchaguzi mapema ili kuhakikisha kwamba tatizo la ukosefu na upungufu wa vifaa katika vituo vya kupigia kura halijitokezi kabisa.

Amesema, suala la elimu ya mpiga kura, Tume italifanyia kazi na kwa bahati mbaya hapa nchini upigaji kura ni suala la hiyari siyo lazima kama ilivyo katika baadhi ya nchi ambazo mshindi anapatikana kutokana na wingi wa kura alizopata.

Pia amesema, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetoa vibali kwa asasi za kiraia 245 nchi nzima kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura juu ya uchaguzi mkuu ambao utafanyika tarehe 28 Oktoba mwaka huu ambapo wananchi watapiga kura kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.