Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.
IMEELEZWA kuwa wagonjwa wanaopelekwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI)wengi wao ni wa ajali za pikipiki maarufu bodaboda ambazo zimeonyesha kuongoza kwa asilimia 70 na matibabu yake kwa wagonjwa hao gharama ni kubwa kuanzia Shilingi milioni 1.5 na kufika hadi shilingi Milioni 30.
Hayo yameelezwa jijini hapa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya mifupa Muhimbili (MOI),Dkt.Respicous Boniface wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekekezaji wa shughuli za taasisi hiyo na mwelekeo wa utekekezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo amesema kumtibia mgonjwa mmoja ambaye amepata tatizo la kuvunjika katika ajali ya bodaboda gharama zake ni kubwa.
Dkt.Boniface amesema Bodaboda hufika MOI wamevunjika mifupa mikubwa wanaumia vichwa hasa ubongo na wengine huwekwa muda mrefu wodi ya wagonjwa mahututi ICU.
“Kama Taasisi tumekuwa tukiwahudumia wagonjwa hawa wa ajali za Bodaboda kwa aliyevunjika mfupa gharama ni Shilingi milioni 1.5 lakini akiumia kichwa akakaa ICU gharama yake ni Shilingi milioni tano hadi sita na akikaa miezi mitatu hapo gharama ndipo inakuwa kubwa hadi kufikia Shilingi Milioni 30,
“Wagonjwa hawa wa ajali za Bodaboda wengi hawana bima na wana hali za chini za kimaisha kwahiyo huwa ni changamoto na kupelekea wengine kutelekezwa wodini na familia zao,”amesema.
Aidha amesema kuwa wagonjwa wengine wengi ambao wamekuwa wakiwapokea ni watoto wenye vichwa vikubwa na migongo wazi.
Akizungumzia utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo na mwelekeo wake Dkt.Boniface amesema kuwa Huduma mpya zilizoanzishwa MOI imeifanya Taasisi hiyo kuokoa fedha nyingi ikiwemo zaidi ya shilingi milioni 608 ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwajili ya kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo.
Ametaja huduma hizo kuwa ni ya kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kupitia tundu la pua (transsphenoidal hypophysectomy)ambapo Wagonjwa 19 wameshafanyiwa upasuaji na gharama za upasuaji huo kwa hapa nchini ni shilingi milioni 8 na nje ya nchi ni Tshs milioni 40 hivyo zingetumika kupeleka wagonjwa hawa nje ya nchi.
“Matumizi ya maabara ya Upasuaji wa Ubongo (angio – suit curthlab)Katika kipindi hiki wagonjwa 186 wamehudumiwa katika maaabara hii gharama za huduma hii hapa nchini ni kati ya Tsh milioni 5-10 na nje ya nchi ni Tsh million 30 mpaka 60 hivyo Taasisi imeokoa kati ya Tsh bilioni 5.6 hadi Tsh bilioni 11.2 ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa hawa nje ya nchi.
Pamoja na hayo amesema kuwa Serikali imekuwa ikitoa fedha kwajili ya kununulia vifaa kwajili ya matibabu ambapo imeshatoa Tsh Bilioni 4.4 kwajili ya ununuzi wa mashine mpya ya kisasa ya MRI na CT scan kwa lengo la kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma hiyo kwa uhakika.
“Taasisi imenunua vifaa vya kisasa, zikiwemo,ICU Ventilators, Monitors, Vitanda na Ambulance ya kisasa vyenye thamani ya tsh. billion 1.3 zilizotolewa na Serikali,”amesema.
Pia amesema Taasisi hiyo imenunua vifaaa vya chumba cha tiba Mtandao vya shilingi milioni 227 kwa ajili ya kuimarisha huduma hiyo nchini pamoja na Ununuzi wa Vipandikizi Serikali imetoa kiasi cha shilingi 4.2 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa ‘Implants’ ili kukabiliana na changamoto la uhaba wa implants kwa wagonjwa.
“Vifaa hivi vimesaidia kuendelea kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa ya Mifupa, Ubongo, Uti wa mgongo na Mishipa ya Fahamu, na hivyo kuokoa maisha ya Watanzania wengi na pesa za serikali ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu Katika kipindi hiki cha mwaka mmmoja jumla ya wagonjwa 7,113 walifanyiwa upasuaji ikilinganishwa na wagonjwa 6,793 waliofanyiwa katika mwaka uliopita wa 2020/2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 2,”amesema Dkt.Boniface.
More Stories
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu