January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MOCSO kuwafikia watoto 315 waishio katika mazingira magumu, Ilemela na Jiji la Mwanza

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Shirika lisilo la serikali la MOCSO lililopo Kiloleli Kata ya Nyasaka wilayani ya Ilemela kupitia mradi wake wa Achieve,limekusudia kuwafikia watoto 315,wanaoishi katika mazingira magumu waliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza.

Ambapo litawafikia kwa kuwapatia mahitaji ya shule kwa lengo la kuwapunguzia gharama wazazi na walezi wao na kuweka mazingira rafiki ya kufanya watoto hao kupenda shule,kupunguza utoro na kuongeza ufaulu wao.

Hayo yamezungumzwa Ofisa Msimamizi Mashauri ya watoto kutoka katika shirika la MOCSO,Amos Jackson wakati wa zoezi la kukabidhi vifaa vya shule vilivyotolewa na shirika hilo kwa ajili ya kuwasaidia watoto wasiojiweza,wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Ambapo wamewapatia sare za shule, soksi, mabegi na mahitaji mengine ya shule ili kuweka mazingira rafiki,salama na waweze kupata elimu bila kikwazo kwa wanafunzi wanaosoma shule za msingi na sekondari zinazopatikana ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza.

“Lengo letu ni kuwafikia watoto hao pamoja na kuisaidia jamii hasa watoto waliopo katika mazingira hatarishi na makundi maalum kwa kupunguza kero na changamoto zinazokwamisha kufikia ndoto zao hasa za kielimu,”ameeleza Amos.

Amos ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa taasisi na mashirika mengine kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na changamoto zinazokabili jamii hasa watoto.

Kwa kuweka mazingira rafiki na salama pia kuja na mikakati inayotekelezeka yenye lengo la kuisaidia jamii dhidi ya changamoto zinazoikabili.

Kwa upande wake Mratibu wa afya shuleni kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Finias Nyaganyi amelipongeza shirika la MOCSO kwa juhudi zake katika kuisaidia serikali katika kupunguza kero na changamoto zinazokabili watoto.

Huku amewaasa wanafunzi walionufaika na msaada huo kutunza na kutumia vizuri vifaa vya shule walivyokabidhiwa ili vikatekeleze lengo lililokusudiwa.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Stella Mbura amewahakikishia watoto kuwa serikali inawajali na itaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuwalinda na kuzuia vitendo vya ukatili kwa watoto huku akiiasa jamii kuripoti na kuchukua hatua katika kudhibiti vitendo vya ukatili.

Mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Nyakato ‘A’ Lucia Bugama,amelishukuru shirika hilo Kwa msaada walioutoa utakaosaidia kuwaondolea adha ya ukosefu wa sare za shule kwani wapo baadhi yao waliokuwa wakishindwa kuhudhuria masomo kutokana na kukosa sare za shule na vifaa vyengine muhimu.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Stella Mbura akimkabidhi sare za shule zilizotolewa na shirika la MOCSO mwanafunzi wa shule ya msingi Gedeli iliyopo Kata ya Nyakato wilayani Ilemela mkoani Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)
Picha ya pamoja ya wanafunzi walionufaika na sare za shule zilizotolewa na shirika la MOCSO.(Picha na Judith Ferdinand)
Mratibu wa Afya shuleni wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Finias Nyaganyi akizungumza na watoto na wazazi waliojitokeza kuchukua sare za shule zilizotolewa na shirika la MOCSO.(Picha na Judith Ferdinand)