April 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mo atakumbukwa si kwa kiasi cha pesa alizopata, bali kwa maisha aliyobadilisha

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline, Dar

MOHAMMED “Mo” Dewji amekuwa mmoja wa wafanyabiashara wenye ushawishi mkubwa
barani Afrika kwa muda mrefu.

Sasa katika hatua mpya ya safari yake ikiwa na ongezeko
kubwa la thamani kati ya dola milioni 400–500 kwa mujibu wa Forbes.

Mo Dewji anatazama mbali zaidi ya ukubwa wa utajiri wake, akilenga kuonesha athari pana za mchango wake katika jamii.

Akiwa mtu wa imani, mfadhili wa kujitolea, na mwekezaji mwenye maono, Mo ana shauku kubwa ya kujenga nafasi za ajira, kupanua biashara zake kimkakati, na kurudisha kwa jamii
kupitia Mo Dewji Foundation (MDF).

Safari ya kujifunza mapema kuwa na utu na kuwajibika
kwa jamii yake hadi kuwa na biashara kubwa ndani ya mabara tofauti tofauti. Anaonesha uongozi wenye kusudi linalovuka mipaka.

Kuangalia Mbele

Mfanyabiashara wa Kimataifa Pamoja na kuthibitishwa kwa ongezeko la thamani ya utajiri wake kwa dola milioni 400–500,
Mo Dewji anabaki kuwa mnyenyekevu kuhusu viwango hivyo vya Forbes.

Kinachomsukuma si hadhi, bali ujumbe wa matumaini na kujitegemea kwa wajasiriamali wa Kiafrika kwa shauku na
utayari wake kuisaidia jamii, mipaka ya kijiografia si kikwazo.

Kampuni ya MeTL Group inaendelea kupanua biashara zake kimataifa, ikiwekeza katika sekta mpya kama teknolojia, mali isiyohamishika na ukarimu, huku ikiimarisha misingi yake katika
kilimo, viwanda, na usambazaji.

Wakati huo huo, shughuli za uhisani wa Mo zinapanuka zaidi kupitia ushirikiano wa kimataifa na taasisi kama Chuo Kikuu cha Georgetown, MDF inaendelea
kuleta athari chanya katika nyanja za afya, elimu, na upatikanaji wa maji safi kwa wale wanaohitaji zaidi.

“Nina mapenzi makubwa na Tanzania,” anasema Mo na kuongeza; “lakini ni wakati sasa wa dunia kutambua kuwa Afrika inaweza kutoa kampuni kubwa za kimataifa, kampuni na viongozi wenye athari ya kweli duniani kote.

Kwa mtazamo sahihi, tunaweza kupeleka maadili yetu ya mshikamano, huruma, na ukarimu katika jukwaa la kimataifa.”

Nguvu ya Kibiashara ya Mabilioni ya Dola

Japo kuwa MeTL Group imejikita Tanzania, mafanikio yake yamevuka mipaka kwa muda mrefu.

Chini ya uongozi wa Mo, MeTL imekuwa mfano wa kampuni inayovuka mataifa, ikiwa na shughuli katika nchi zaidi ya 11 za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Kila soko jipya linaongeza mapato ya kampuni, kupunguza utegemezi kwenye uchumi mmoja pekee.

“Kutawala soko la ndani ilikuwa hatua ya kwanza,” anasema Mo, akieleza jinsi MeTL inavyochangia zaidi ya asilimia 3 ya Pato la Tanzania.

“Lakini kubaki hapo ni kujizuia kuongezeka. Dira yetu daima ilikuwa Afrika nzima na hatimaye dunia nzima.”Anasema

Dira hiyo sasa ni ukweli, MeTL inasafirisha bidhaa zake kuanzia nyuzi za mkonge hadi bidhaa za walaji katika masoko ya Mashariki ya Kati, Asia, na Ulaya.

Kupitia vituo vyake vya biashara huko Dubai, Mo anahakikisha mtiririko mzuri wa bidhaa na mitaji, akiamini kuwa “haitoshi kufanikiwa nyumbani pekee, ni lazima uangalie nje ya nchi pia.” Leo, MeTL ni kampuni yenye nguvu ya Kiafrika yenye uwepo wa kimataifa unaoanzia Kenya, Uganda, Msumbiji, Zambia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, hadi India, Thailand, Italia, Vietnam, na kwingineko.

Zaidi ya Tanzania na Afrika

Baada ya utekaji wake mnamo 2018 na siku tisa za kutekwa, Mo Dewji alitoka akiwa na maono mapya akiongeza kasi ya upanuzi wa biashara zake kimataifa na kujikita zaidi katika ujasiriamali wenye matokeo chanya.

Hili limechangia ongezeko la thamani ya utajiri wake hadi
kufikia zaidi ya dola bilioni 2.3. “Sitaweza kufanikiwa kwa kutegemea Afrika pekee,” anafafanua Mo Dewji na kusisitiza;

“Afrika ni nyumbani, lakini tunastawi pia Asia, Mashariki ya Kati, na Ulaya popote tunapoona fursa tunaichangamkia ili kuleta uvumbuzi wenye tija.”

Mwelekeo wake sasa unaongezeka hadi kwenye sekta za mali isiyohamishika, ukarimu, usindikaji taka, na teknolojia ya fedha (FinTech)—sekta zinazokamilisha nguzo zake zilizopo za
viwanda vya chakula, utengenezaji, na biashara ya rejareja.

Kwa kusimika falsafa yake ya athari za kijamii ndani ya biashara hizi, Mo Dewji anathibitisha kuwa uwekezaji makini unaweza kuleta manufaa makubwa kwa jamii ndani na nje ya Tanzania.

Ajira na Maendeleo ya Jamii

Mo anajulikana kwa kuwekeza katika sekta ngumu kama viwanda vya nguo na kilimo, ambavyo mara nyingi huepukwa kwa sababu ya hatari zake.

Kwa kutambua fursa zilizokuwa hazijatumika, aliokoa mashamba ya mkonge yaliyokuwa yameachwa, akieleza kuwa “uzalishaji wa nyuzi za mkonge kwa kiwango kikubwa ni kama kuchapisha pesa.”

Vivyo hivyo, alianzisha Mo Cola kushindana na ‘majitu’ ya kimataifa ya vinywaji baridi, akihamasisha uzalishaji wa ndani
wa bidhaa zinazotegemewa kutoka nje.

Lakini kwa Mo, mafanikio hayapimwi kwa faida pekee yanapimwa kwa athari kwa jamii.

“Kitu cha maana zaidi ni athari unayoacha kwa jamii, nafasi za ajira unazounda, na maisha unayogusa.”

Sekta ya michezo

Mchango wa Mo Dewji si katika biashara na uhisani pekee, bali pia kwenye soka la Tanzania kupitia klabu ya Simba SC.

Amebadilisha Simba SC kuwa Klabu ya kiwango cha Juu Afrika.

Kama Rais na mwekezaji mkuu, amesimamia mageuzi makubwa yaliyoipeleka Simba SC kutoka nje ya nafasi 100 bora hadi nafasi ya 7 barani Afrika.

Mabadiliko aliyoyaongoza ni makubwa kutoka kwa mchakato wa kuirebrand klabu na kutambulisha nembo mpya hadi kuhakikisha wachezaji wanalipwa mishahara rasmi.

Mo alihakikisha kuwa wachezaji hawapati tena mishahara midogo ya sh. 50,000, bali wanahamasishwa kwa mazingira bora ya kazi yao.

“Mpira si kuhusu kushinda pekee; ni kuhusu kuhamasisha vijana na kutoa fursa zinazoleta mabadiliko ya kweli,” anasema Mo.

***Uhisani wa Maisha

Mo Dewji Foundation & The Giving Pledge Mo Dewji ameahidi kutoa nusu ya utajiri wake kwa misaada, akifuata mafundisho ya imani yake. Kupitia MDF, ameleta mabadiliko makubwa kwenye afya, elimu, na upatikanaji wa maji safi kwa jamii za pembezoni.

“Nilifundishwa na wazazi wangu kuwa uhisani ni wajibu, si chaguo,” anasema Mo Dewji.

Mo Dewji ameonesha kuwa biashara inaweza kuwa chombo cha mabadiliko chanya kutoka kujenga viwanda na kuzalisha ajira hadi kusaidia jamii kupitia uhisani.

“Ninataka nikumbukwe si kwa kiasi cha pesa nilichopata, bali kwa maisha niliyo badilisha,” anasema Mo Dewji.