Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOline,Muheza
MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Timotheo Mnzava amewataka wananchi wa Kijiji cha Ubembe, Kata ya Nkumba, Wilaya ya Muheza mkoani Tanga kuheshimu Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa kuhakikisha hawazalishi migogoro kwa wakulima na wafugaji.
Amesema Serikali inatumia fedha nyingi katika kupanga matumizi ya ardhi, nia ikiwa ni kuona wananchi wanafanya shughuli zao za kiuchumi kwa amani, hivyo na wao wanatakiwa kuiunga mkono kwenye mpango huo.
Ameyasema hayo Machi 16, 2026 wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilipofika Kijiji cha Ubembe kuona Utekelezaji wa Mradi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi wa kijiji hicho.
“Watu wa Ubembe ni lazima tuwakumbushe, kufanya mipango ya matumizi ya ardhi ni jambo moja, kuiheshimu na kuisimamia ni jambo jingine. Ni maombi na wito wetu kwenu, kazi hii nzuri iliyotumia fedha nyingi za walipa kodi ikiwemo ninyi wenyewe wana Ubembe, ili iwe na maana na faida ni ninyi kuheshimu mipango mliojiwekea wenyewe. Hatutarajii kusikia baada ya mpango huu kuna mkulima anakwenda kulima sehemu ya kuchungia.
“Na hatutarajii kuona mfugaji ama mchungaji, anakwenda kuchunga maeneo ya kilimo, na wala hatutatarajia kuona mkulima anakwenda kulima maeneo yaliyotengwa ikiwemo vyanzo vya maji. Kwa kuwa na mpango huu kila mmoja akaishi na kufanya majukumu yake kutokana na mpango wa matumizi ya ardhi tulioutengeneza wenyewe, na tuliokubaliana wenyewe” amesema Mnzava.

Mnzava amesema, Mbunge wa Jimbo la Muheza Hamis Mwinjuma maarufu kama MwanaFA, pamoja na kuipongeza Serikali kuweza kuweka Mipango ya Matumizi ya Ardhi, ameomba wananchi kwenye vijiji hivyo wapewe Hakimiliki ya Kimila, kwani itawasaidia kuweza kufanya shughuli zao kwa uhakika, na kuzitumia hati hizo kufanya shughuli za maendeleo.
“Ili kazi hii iwe na maana zaidi, sisi kama Kamati tunaitaka Wizara kumalizia zoezi hili kwenda kwenye hatua ya kutoa Hakimiliki ya Kimila, ili wananchi wa kijiji hiki wapate Hatimiliki ya Kimila ili wawe na umiliki unaoeleweka wa ardhi yao, na pia hati hizo watazitumia kwa mambo yao mengine.
“Lakini jambo jingine ambalo Mwinjuma ametuomba ni kuwa kati ya vijiji vyake 126 vya Wilaya ya Muheza, ni vijiji 46 tu ndivyo vipo kwenye Mipango ya Matumizi ya Ardhi, hivyo vijiji vingine 80 kuwa nje ya mpango huo. Na hata Diwani wa Kata ya Nkumba amesema kati ya vijiji vyake vitano, ni kijiji kimoja ndicho kimo kwenye mpango huo, hivyo tunaomba awamu inayokuja Tume iongeze vijiji vingine Jimbo la Muheza, na kipaumbele kwenye Kata ya Nkumba” amesema Mnzava.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ubembe, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Tume ya Taifa ya Mipango ya
Matumizi ya Ardhi iliidhinishiwa sh. 2,520,616,000 kwa ajili ya
utekelezaji wa Mradi wa Upangaji wa Matumizi ya Ardhi. Aidha, katika
kipindi cha mwezi Desemba, 2025 na Februari, 2026, Tume iliongezewa
sh. bilioni mbili hivyo kuwa na bajeti ya sh. 4,520,616,000.
Mmuya amesema lengo lilikuwa ni kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa vijiji 240, kuandaa mipangokina ya makazi na mashamba katika vijiji 10, kutoa Hati za Hakimiliki za Kimila 2,000 na kufanya ufuatiliaji na tathmini. Hadi
Februari 2026, Wizara kupitia Tume imepokea fedha sh. 4,520,616,000
sawa na asilimia 100.
“Fedha hizi zimetumika kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 191 sawa na asilimia 79.58 ya vijiji 240 vilivyopangwa hivyo kufikia idadi ya vijiji vilivyoandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi kufikia 4,873 (asilimia 39.50) kati ya vijiji 12,333 vilivyopo nchini. Kati ya vijiji hivyo, vijiji 2,697 (asilimia 55.35) vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan” amesema Mmuya.
Naye Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUPC) Joseph Mafuru amesema utekelezaji wa mradi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza umechangia kuwa na vijiji 357 (46.79%) vilivyo na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya
vijiji kati ya vijiji 763 vilivyopo katika Halmashauri za Wilaya nane (8) zilizopo Mkoa wa Tanga.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza utekelezaji wa mradi huo
umefanyika kwa kuandaa mipango ya Matumizi ya ardhi ya vijiji nane (8)
vya Mindu, Lunguza, Mkuzi, Mgome, Mpapayu, Ubembe, Misongeni na
Enzi. Idadi hii inakamilisha kuwa na jumla ya vijiji 46 (asilimia 36.51)
vyenye mipango ya Matumizi ya Ardhi kati ya vijiji 126 vilivyopo katika
Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
” Aidha, vijiji vitano (5) vya Kigombe,
Kicheba A, Kicheba B, Bombani na Kwabada vimetangazwa kuwa maeneo ya kuendelezwa kimji chini ya Sheria ya Mipangomiji, Sura ya 355.
Mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vinane (8) imewezesha kutengwa
kwa maeneo ya matumizi mbalimbali. Matumizi hayo ni Makazi hekta
563.34, Makazi na Kilimo hekta 1, 750.03; Kilimo hekta 3,596.64; Hifadhi
za Misitu ya Vijiji hekta 5.23; Huduma za Jamii hekta 46.36; Maeneo ya
uwekezaji hekta 8.22; Hifadhi ya Vyanzo vya Maji hekta 36.17; Hifadhi za Miundo mbinu ikiwemo Barabara na Umeme hekta 160.92 na nyinginezo.
“Kijiji cha Ubembe ni mojawapo kati ya vijiji vinane (8) vilivyoandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza. Utekezaji wa kazi za upangaji wa matumizi ya ardhi ulifanyika katika Kijiji cha Ubembe Januari, 2026 kwa kushirikisha jamii kupitia vikao vya Serikali ya Kijiji na mikutano ya wananchi pamoja na utoaji wa mafunzo kwa wajumbe wa
Serikali ya Kijiji (VC), Kamati ya Usimamizi wa Matumizi ya Ardhi (VLUMC) na Baraza la Ardhi la Kijiji ( BLAK)” amesema Mafuru.


More Stories
77 mbaroni tuhuma za kuhujumu miundombinu ya reli
Chanjo ya polio kuwafikia watoto 146,960 Ilemela
Ilemela yatoa mikopo kwa vikundi 41