January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MNEC Simiyu atimiza ahadi alioitoa mbele ya Makonda

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Busenga

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa Mkoa wa Simiyu (MNEC), Emmanuel Gungu Silanga ametimiza ahadi yake aliyoitoa mbele ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Paul Makonda ya kununua Baiskeli kwa ajili ya mtu mwenye ulemavu ambaye aliomba msaada huo katika ziara ya Mwenezi huyo katika Kata ya Lamadi wakati akielekea mkoani Mara.

Akizungumza na Mabalozi wa CCM Kata ya Lamadi mkoani Simiyu alipofika kwa lengo la kukabidhi msada huo, Gungu amesema katika ziara hiyo ya Mwenezi wa Taifa walijitokeza watu wengi kuomba misaada na walisaidiwa hapo hapo.

“Katika ziara ya Mwenezi Makonda wakati anaelekea mkoani Mara kwenye ziara yake ya kikazi kama mnakumbuka kuna mwenzetu mmoja alijitokeza nakuomba msaada wa Baiskeli ili kumuwezesha kufanya shughuli zake, mimi nilisema nitampa na leo nimeileta kuikabidhi,”amesema Gungu.

Aidha, Gungu amewataka mabalozi wa CCM kuchapa kazi, kwani chama kinatambua kazi kubwa wanazofanya na kwamba ataketi nao pamoja baada ya Mabalozi wa Jimbo la Busega kumuomba wakae nae kwani wanamambo mengi ya kumwambia.

Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Busega, Kauli Idaso Mayala amemshukuru Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu CCM Taifa kwa kutimiza ahadi yake na kueleza kuwa baiskeli( kiti mwendo)hiyo itamfikia mlengwa mara moja.

“Tunakushukuru sana Mheshimiwa Mnec kwa moyo wako wa upendo katika ziara ya Mwenezi wetu wa Taifa Makonda uliahidi hapa Lamadi na umetekelza,leo kwa furaha tunapokea baiskeli hii nikuhakikishie itamfikia muhusika mara moja,”amesema Idaso.

Mkuu wa Wilaya ya Busega, Anna Gidarya alimkabidhi baiskeli hiyo mlemavu huyo, John Chalres kwa niaba ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Emmanuel Gungu Silanga.