Na Esther Macha, Timesmajira Online , Mbeya
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (MNEC), Ndele Mwaselela, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka siasa za maendeleo zinazogusa maisha ya wananchi wa kawaida na kumjali mtu wa chini.
MNEC Mwaselela, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Paradise Mission and Patrick, aliyasema hayo Januari 16, 2026, wakati akikabidhi meza na viti 400 kwa Shule ya Sekondari ya Malawa, iliyopo Kitongoji cha Mapinduzi, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Vijijini. Msaada huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 ya Shule ya Paradise Mission iliyopo Kata ya Nsalala.
“Tunahitaji siasa zitakazokuwa mkombozi kwa kumhurumia mnyonge aliyepo chini. Siasa zinazogusa maisha ya wananchi kwa vitendo. Kujenga vyoo shuleni ni kupunguza adha kwa watoto wetu, kutoa meza na viti ni kupunguza mateso kwa wanafunzi. Mkuu wa shule amesema wanahitaji meza 600; mimi nitaongoza wenzangu kuhakikisha mwaka huu Kata ya Nsalala haina upungufu wa meza wala viti,” amesema Mwaselela.
Ameongeza kuwa atakutana na viongozi na wadau mbalimbali ili kuhakikisha changamoto zilizopo zinatatuliwa, akisema ni aibu kwa viongozi kufanikiwa kimaisha ilhali watoto wanasoma katika mazingira duni.
“Hatupaswi kusema kila wakati tunataka Rais Samia aje kutatua kila changamoto. Tayari ametuteua sisi. Ni jukumu letu kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi na serikali vinang’ara kwa kutekeleza miradi na kutatua kero za wananchi,” amesema.
Mwaselela amesema jukumu kubwa la viongozi ni kuwaeleza wananchi kuwa chama kina nguvu kwa kuzungumza na kutekeleza maendeleo yaliyopo kwa vitendo.

Akitoa mfano wa mchango wake wa awali katika jamii, amesema mwaka 2018 alijenga darasa katika Shule ya Iyela akiwa hana cheo chochote, na baadaye kujenga vyoo mwaka 2019.
“Mimi ni mwanasiasa ninayefanya kazi kwa vitendo. Sijaanza kuhudumia jamii leo, nina zaidi ya miaka 14 nikitoa huduma. Nimekula kiapo cha kugusa maisha ya wananchi,” amesema.
Amesema pia anatamani kuona wanawake mama lishe wakinufaika kiuchumi na watoto wao wakipata fursa kubwa, akisisitiza kuwa uteuzi wa Rais Samia kwa mtoto wa mama lishe hadi nafasi ya UNEC ni ishara kuwa kila Mtanzania ana nafasi ya kufanikiwa.
Kwa upande wake, Aliko Mbuba, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, amesema halmashauri hiyo imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa samani shuleni, hususan meza na viti.
“Malezi na elimu bora haviwezi kupatikana bila mwanafunzi kuwa na mahali pa kukaa na kuandikia. Tunampongeza MNEC kwa kusimamia maelekezo ya Rais kuwa kila mwanafunzi akae kwenye kiti,” amesema Mbuba.
Naye Neema Mwakimenya, Mkuu wa Shule ya Sekondari Malawa, amesema shule hiyo ina upungufu wa matundu 16 ya vyoo kwa wanafunzi wa kiume, huku upande wa wasichana ukiwa na vyoo vya kutosha.
Ameongeza kuwa shule ina upungufu wa samani 673, na kwamba msaada wa meza na viti 400 uliotolewa na MNEC Mwaselela umepunguza kwa kiasi kikubwa mzigo uliokuwepo.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi