Mbunge Christina Mndeme Asisitiza Nishati Safi ya Kupikia Katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050
Na Joyce Kasiki,Dodoma
MBUNGE wa Viti Maalum, Christina Mndeme, amechangia mjadala wa Mipango ya Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 kwa kusisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza na kupanua matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususan kwa wanawake na wananchi waishio vijijini.
Mbunge Mndeme alisema kuwa wanawake wa Mkoa wa Tabora walimpa kura za imani zilizomwezesha kuwa mwakilishi wao Bungeni, na akaahidi kuendelea kupigania maslahi yao, hususan katika nyanja za afya, uchumi na mazingira.
Akizungumza Bungeni, Mndeme alisema ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeleta mafanikio makubwa, ambapo idadi ya watumiaji wa nishati safi ya kupikia imeongezeka kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 23.2 kwa sasa.
Katika mchango wake, alimpongeza Rais Samia kwa kutoa ruzuku ya asilimia 50 kwa mitungi 452,445 ya gesi ya kilo 6, pamoja na ruzuku ya asilimia 85 kwa majiko banifu 200,000, hususan kwa wananchi wanaoishi vijijini, ambapo wanufaika wakubwa ni wanawake.
“Mhe. Spika, nishati safi ni uchumi, nishati safi ni afya, na nishati safi ni mazingira. Naomba tuendelee kupanua wigo wa elimu ya matumizi ya nishati safi kwa wananchi, kama ilivyoelekezwa katika Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia uliozinduliwa na Rais Samia mwezi Mei 2024,” alisema Mndeme.
Aidha, alishauri kuongezwa kwa upatikanaji wa majiko ya gesi na majiko banifu yenye ruzuku, huku akizipongeza taasisi 1,136 zilizoitikia wito wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa vitendo.
Hata hivyo, alisema bado zipo taasisi ambazo hazijaunga mkono juhudi hizo, na akashauri kuwekwa kwa sheria, kanuni na miongozo itakayolazimisha taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ya kupikia.
“Isiwe hiari tena, bali iwe ni lazima kwa mujibu wa sheria na taratibu, ili kulinda mazingira yetu,” alisisitiza.
Mbunge huyo alibainisha kuwa kwa sasa kaya zipatazo 2,000 zinatumia gesi asilia kwa ajili ya kupikia, na akashauri kuongezwa kwa wigo wa matumizi ya gesi asilia majumbani.
Pia alitoa wito wa kuongezwa kwa uwekezaji katika nishati safi ya kupikia, kupunguzwa kwa tozo na kodi kwenye nishati na teknolojia za nishati safi pamoja na mashine za kutengeneza majiko hayo ili yaweze kupatikana kwa bei nafuu.
Vilevile, alishauri kuanzishwa kwa teknolojia ya “Pay As You Use”, ambapo mtumiaji hulipa kulingana na kiasi cha gesi anachotumia, sambamba na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kuongeza uwekezaji zaidi katika sekta ya nishati safi ya kupikia.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria