Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Dar
Wazazi na walezi nchini wametakiwa kurudi kwenye misingi ya malezi ili kuwaepusha watoto dhidi ya mmomonyoko wa maadili unachagizwa na athari ya kukua kwa teknolojia.
Hali hiyo imebainika wakati Mahafali ya kidato cha sita ya shule ya Sekondari Mtakatifu Joseph Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam walipokua wakiwasilisha risala yao kwenye mahafali ya 12 ya shule hiyo Mei 20, 2023.
Wahitimu Kersten Mbuligwe na Nancy Kitena wamesema changamoto ya kukua kwa teknolojia imewaathiri vijana wengi hali inayochangia mmomonyoko wa maadili kushamiri ndani ya jamii.
“Ili kukabiliana na changamoto hii ni lazima wazazi na Jamii warudi katika misingi ya malezi shirikishi ili kuwalea watoto vema, viongozi wa Dini wanatakiwa kutoa mafundisho ya malezi bora na kuwalea watoto kwenye misingi ya dini, vilevile tunaiomba Serikali iweke sheria kali dhidi ya wanaokiuka maadili” amesema Mbuligwe.
Akizungumza na wahitimu, wazazi na wanafunzi wa shule hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesisitiza umuhimu wa wazazi kutoa huduma muhimu kwa watoto wao ikiwemo kuwaepusha na madhara ya utandawazi na kuiga tamaduni za watu wengine.
“Serikali imekuwa ikifanya kampeni mbalimbali za kuwakutanisha makundi ya watu kwenye jamii kwa ajili ya kutoa elimu dhidi ya ukatili, malezi chanya, haki za watoto na umuhimu wa kuzingatia maadili mema” amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima Ameongeza kuwa tatizo la mimba za utotoni bado ni kubwa na linazorotesha maendeleo ya masomo kwa watoto wa kike ambapo amesema utafiti wa Afya ya uzazi kwaa mtoto na viashiria vya Malaria ya mwaka 2015/16 kuwa asilimia 27 ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15-19 wamepata ujauzito katika mikoa ya Katavi, Tabora, Dodoma, Morogoro na Mara.
Dkt. Gwajima amewaasa wahitimu kuwa chachu ya mabadiliko kwenye jamii baada ya kuhitimu masomo yao kwa kuhakikisha wanazingatia maarifa na kuyatumia yale yote waliojifunza.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo Sista Theodora ametoa rai kwa Serikali na wadau wote kutazama suala la malezi kwa upana wake na umuhimu mkubwa.
“Ili kusaidia, tunashauri kuanzishwa kwa somo la maadili kuanzia elimu ya awali, ukitazama hivi sasa mitaala yetu ni kama hakuna somo linalowasaidia watoto kufahamu tunu za msingi” amesema Sista Theodora.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu