December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mloganzila yapokea darubini ya kufanyia upasuaji

Mwandishi wetu ,TimesMajira Online,Dar es Salaam

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imepokea msaada wa mashine ya upasuaji wa macho (Operating Microscope) yenye thamani ya takribani Sh .milioni 41 kutoka Taasisi ya Vision Care inayojihusisha na mapambano dhidi ya matizo ya upofu duniani.

Msaada huo unalenga kuisaidia hospitali kuendelea kutoa huduma bora na za ubingwa wa juu kwa wagonjwa wanaokabiliwa na matatizo ya macho wanaofika kupatiwa matibabu hospitalini hapa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru    ameishukuru taasisi hiyo kwa kuendeleza mahusiano pamoja na kuunga mkono juhudi za hospitali katika kuboresha huduma za afya kwa kutoa mashine ambayo itasaidia utoaji wa huduma bora katika Idara ya Magojwa ya Macho.

“Msaada huu umekuja wakati muafaka ambapo tunauhitaji wa mashine kama hii ambayo itatusaidia kuongeza tija katika huduma zetu hasa idara ya Magonjwa ya Macho,tunawashukuru sana  kwa ushirikiano wenu katika kusaidia kuboresha huduma za afya”amesema Prof. Museru.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Macho Muhimbili-Mloganzila, Catherine Makunja amesema mashine ya upasuaji wa macho (Operating Microscope) ni muhimu kwani kila mgonjwa anayehitaji kufanyiwa upasuaji wa jicho lazima mashine hiyo itumike.

“Jicho ni kiungo kidogo ambacho upasuaji wake unahitaji umakini wa hali ya juu na Operating Microscope ndio mashine pekee ambayo itamsaidia daktari kufanya upasuaji”amesema Dkt. Makunja 
Kwa mujibu wa Dkt. Makunja tatizo la macho limeongezeka kwa sasa kutokana na madiliko ya mfumo wa maisha ambapo katika Kliniki ya Magonjwa ya Macho Mloganzila wagonjwa 350 hadi 400 huonwa kwa mwezi na baadhi yao wanahitaji kufanyiwa upasuaji.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Vision Care Bi. Jihye Kim amesema wanayofuraha kukabidhi msaada huu ambao utasaidia wataalamu kufanya kazi kwa ufanisi na kuahidi kuendeleza mahusiano ili kuendelea kuboresha huduma. 
Februari mwaka huu Taasisi ya Vision Care pia ilikabidhi msaada wa mashine ya uchunguzi wa macho (Slit Lamp Biomicroscope ) yenye thamani ya takribani TZS. 20Mil.