January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mlawa aipiga tafu TaSUBa vifaa vya michezo

Na Omary Mngindo, TimesMajira Online, Bagamoyo

MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, Aboubakary Mlawa, ameipatia seti mbili za jezi Taasisi ya Sanaa na Utamaduni TaSUBa ili kuendeleza shughili za michezo.

Mlawa amekabidhi seti hizo katika Mahafali kwa wanachuo 59 waliohitimu masomo yao, ambapo katika taarifa ya wahitimu hao iliyosomwa na Anjela Mhilu iligusia changamoto mbalimbali zinazokabili katika eneo hilo la michezo.

Amesema, taasisi hiyo ni kubwa na ina heshima kubwa ndani ya nchi na hata Afrika Mashariki na Kati, kwani imekuwa na mchango mkubwa kwenye sanaa hivyo anaamini jezi hizo zitasaidia kuwapatia fursa wanafunzi na watumishi kushiriki michezo.

“Katika taarifa yenu nimesikia mna upungufu wa vifaa kama kompyuta, printa, fotokopi na vifaa mbalimbali vya sanaa ikiwemo ngoma, hili nalichukua nitanunua na kuwakabidhi kwani nimeona mmesema mnataka kumuunga mkono kwa vitendo Dkt. John Magufuli hivyo sisi Jumuia ya Wazazi tupo pamoja nanyi,” amesema Mlawa.

Amesema, anatambua umuhimu wa chuo hicho kwani wakati anasoma elimu ya sekondari Bagamoyo alikuwa anafika chuoni hapo kujionea namna wanachuo wanavyoshiriki sanaa hiyo.

Kwa upande wake, rais wa chuo Richard Mtambo amesmhukuru Mlawa kwa kuonesha kugushwa na changamoto hizo, na kusema kuwa wamefurahishwa na hatua ya kupokelewa kwa changamoto inazoikabili chuo.

Mgombea udiwani Kata ya Dunda ilipo taasisi hiyo Apsa Kilingo ameahidi kuwakabidhi seti ya jezi za netiboli, wakati Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi Kata hiyo Haji Fuko akiahidi kutoa mipira minne.