Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online ,Geita
MKUU wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, ameipongeza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kwa kuja na wazo la kuanzisha mradi mkubwa wa Makazi ya Biashara mkoani Geita, akisema ni hatua muhimu katika kutafsiri kwa vitendo maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Bi. Kingalame alitoa pongezi hizo alipofanya ziara katika banda la TBA kwenye Maonyesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili, mkoani Geita.
“Nimefurahishwa sana na mpango huu wa TBA. Mradi huu wa Makazi ya Biashara ni tafsiri halisi ya maono ya Rais wetu Dkt. Samia, ambaye anatamani kuona Watanzania wanaishi kwenye makazi bora, salama na ya kisasa,” alisema Bi. Kingalame.
Aidha, alitoa wito kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa hiyo kwa kushirikiana na TBA katika kuhakikisha ujenzi wa makazi hayo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
“Naipongeza TBA kwa kukaribisha sekta binafsi kwenye mradi huu. Hii ni fursa adhimu kwa sekta binafsi kuwekeza, kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto ya makazi bora kwa watumishi na wananchi kwa ujumla,” aliongeza.
Akisisitiza umuhimu wa mradi huo, Mkuu huyo wa Wilaya alisema makazi hayo yataleta faraja kubwa kwa wananchi wa Geita, kwani yatachangia kuboresha maisha na mazingira ya kuishi kwa familia nyingi, pamoja na kuongeza mvuto wa mji wa Geita kimaendeleo.
“Hii ndiyo tafsiri ya dhamira njema ya Rais wetu – kuona wananchi wake wanaishi katika mazingira mazuri, salama na yenye hadhi. Tunapongeza TBA kwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa dhamira hiyo,” alisisitiza Bi. Kingalame.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi