


Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma
MKUU wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele, amewatoa hofu wazazi na walezi kuhusu mafunzo ya JKT, akisisitiza kuwa ni sehemu salama ya malezi ya vijana kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Meja Jenerali Mabele alisema kuwa kumekuwepo na taarifa potofu zinazozunguka mitandaoni zikidai kuwa mafunzo ya JKT ni ya kutesa vijana, jambo alilolikanusha vikali.
”Mafunzo ya JKT ni ya kujenga nidhamu, maadili, uaminifu, utiifu na moyo wa kazi kwa vijana wetu,” alisema.
Aliongeza kuwa JKT ina utaratibu mzuri wa malezi unaoshirikisha kamati maalum zinazofuatilia hali ya kijamii ya vijana wakati wa mafunzo.
”Kama kijana amepata changamoto yoyote, kuna njia rasmi za kutoa taarifa na hatua huchukuliwa mara moja,” alisisitiza
Meja Jenerali Mabele alisema kuwa hadi sasa miundombinu ya JKT ipo imara na tayari kuwapokea vijana hadi 60,000 kwa mwaka, na akawahimiza wazazi kuacha woga na kuwahimiza vijana wao kujiunga na mafunzo hayo.
”JKT siyo mahali pa kuteseka, bali ni darasa muhimu la maisha,” alisema.
Kwa upande mwingine, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Profesa LughanonKusiluka ameungana na Mkuu wa JKT akieleza kuwa wanafunzi waliopitia mafunzo ya JKT wameleta mabadiliko chanya chuoni hapo.
”Tumeshuhudia utulivu, usikivu na nidhamu ya hali ya juu kwa wanafunzi waliopitia JKT,” alisema Prof Kusiluka
Katika kikao cha serikali ya wanafunzi wa UDOM, baadhi ya viongozi waliowahi kupitia JKT walielezea jinsi gani mafunzo hayo yamewajenga katika kujiamini, kuongoza na kufanya kazi kwa bidii.
Noel Mtikita, Mkuu wa Itifaki wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo, alisema: “JKT imetufundisha nidhamu, uzalendo, na ujasiriamali. Tuna uwezo mkubwa wa kuongoza kwa sababu tuliandaliwa vizuri.”
Naye Katibu wa Fedha wa serikali hiyo, Frolentino Kamiguzi, alisema: “Uongozi si kazi rahisi, bila mafunzo ya JKT, huwezi kujitambua vizuri. Tunaomba vijana wasidanganywe na maneno ya mitandaoni bali waende wakajifunze mafunzo haya ya msingi.
Kwa sasa, nafasi za kujiunga na JKT kwa mujibu wa sheria zimetangazwa rasmi ambapo wanafunzi wa kidato cha sita waliohitimu mwaka huu wanahitajika kuripoti katika kambi mbalimbali wakiwa na vifaa vilivyotangazwa.
More Stories
Vyombo vya habari vyatakiwa kuzingatia weledi kuelekea uchaguzi mkuu
Jeshi la Polisi lawataka wahalifu kukaa chonjo kwa walemavu
TANESCO yashinda tuzo ya uhifadhi mazingira kupitia mradi wa JNHPP