Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Shirika la Kilimo Hai Tanzania (TOAM), kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, limetangaza kuahirishwa kwa Mkutano wa Nne wa Kitaifa wa Kilimo Ikolojia Hai (IV NEOAC) ambao sasa utafanyika kuanzia Machi 03 hadi 05, 2026 katika Jiji la Dodoma.
Awali mkutano huo ulipangwa kufanyika Januari 27 hadi 29, 2026, lakini umeahirishwa ili kuimarisha maandalizi na kuruhusu ushiriki mpana wa wadau muhimu.
Akizungumza kuhusu mabadiliko hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TOAM, Bakari Mongo, alisema uamuzi wa kuahirisha mkutano umezingatia ubora na tija ya tukio hilo.
“Tunashukuru kwa uvumilivu na uelewa wa wadau wetu. Tarehe hizi mpya zinatupa fursa ya kuandaa mkutano ulio bora zaidi, wenye programu iliyoimarishwa itakayonufaisha Kilimo Ikolojia Hai nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla,”amesema Mongo.

“Toam radhi wadau wote kwa usumbufu wowote uliotokana na mabadiliko ya tarehe, na imewahakikishia kuwa maandalizi yanaendelea ili kuhakikisha mkutano unakuwa na matokeo chanya na ya kudumu. Taarifa zaidi kuhusu programu iliyosasishwa, wasemaji na usajili zinapatikana kupitia tovuti rasmi ya mkutano.”
Mkutano wa IV NEOAC unatarajiwa kuwakutanisha wadau takribani 400 wakiwemo wakulima, watunga sera, watafiti, wasomi, sekta binafsi, vyama vya kiraia, wabia wa maendeleo pamoja na wanahabari. Washiriki watapata fursa ya kubadilishana maarifa na uzoefu kwa lengo la kuimarisha mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula, kulinda mazingira na kuongeza kipato cha wakulima wadogo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi wa Mtandao wa Mwamvuli wa Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Mwatima Juma, amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu kwa mustakabali wa kilimo endelevu nchini.
“IV NEOAC ni fursa adhimu ya kitaifa ya kuimarisha mijadala ya sera, teknolojia na mifumo ya uzalishaji wa chakula endelevu, huku tukikabiliana kwa pamoja na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na usalama wa chakula,” alisema Mwatima Juma.
Maudhui makuu ya mkutano huo ni “Kilimo Ikolojia Hai kwa Mifumo Endelevu ya Chakula”, ambapo majadiliano yataangazia usalama wa chakula na lishe, mbinu na teknolojia za Kilimo Ikolojia Hai, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, manufaa ya kiuchumi kwa wakulima pamoja na mazingira ya kisera katika kuendeleza sekta hiyo.

Naye Gladness Martin, Mwakilishi wa SWISSAID Tanzania na mdhamini wa mkutano huo, amesema kuwa wameungana kwa pamoja na kukubaliana kuwa kuhairishwa kwa mkutano huo ni mpango wa kuandaa tukio hilo kwa ukubwa zaidi.
Ameongeza kuwa, kutokana na umuhimu mkubwa wa mkutano huo, wameona ni vyema kuchangia jitihada za kuutangaza ndani na nje ya nchi, hususan katika kuibua na kujadili masuala ya kilimo.

Aidha, amesema wanatambua na kuthamini juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza sekta ya kilimo na kuimarisha mazingira ya mijadala ya maendeleo.
Charles Bupamba, Mwanachama wa Taasisi ya TOAM, amewaomba wadau kuongeza bidii katika kufuatilia na kuelewa kwa kina masuala ya kilimo hai, pamoja na kushiriki katika kongamano hilo ili kupata fursa ya kujifunza kwa undani elimu ya kilimo na kueneza maarifa yote yanayohusiana na sekta ya kilimo.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi