Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Kahama
Mjumbe wa Taifa wa Kamati Tendaji Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Azan Mufti, amesema mkutano mkuu wa shirikisho hilo unatarajiwa kufanyika Februari 28, mwaka huu wilayani Kahama mkoani Shinyanga.
Mufti ambaye pia ni mjumbe wa mkutano mkuu wa TFF kutoka Mkoa wa Shinyanga, ametoa taarifa hiyo Februari 20,2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Kahama.
Amesema maandalizi ya mkutano huo yanaendelea vizuri huku TFF ikichagua Kahama kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu katika kalenda ya mpira wa miguu nchini.
Ameeleza kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wataanza kuwasili wilayani Kahama kuanzia Februari 21, tayari kwa kushiriki kikao hicho kitakachojadili masuala mbalimbali ya maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Mufti amewakaribisha wanamichezo, wadau wa michezo pamoja na wananchi wa Kahama na maeneo ya jirani kujitokeza kwa wingi kuwapokea wajumbe hao kwa shangwe na ukarimu wa hali ya juu, na kuhakikisha wanakuwa wenyeji wema hadi watakapoondoka baada ya kukamilika kwa mkutano huo.
Amesisitiza kuwa kufanyika kwa mkutano huo Kahama ni fursa kwa wakazi wa eneo hilo kushuhudia na kushiriki kwa karibu katika maamuzi na mwelekeo wa maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania.
Amesema Februari 25,2026, Rais wa TFF pamoja na Makamu wake wataanza kwa kufanya kikao cha kuongea na wanamichezo na wadau wa michezo wilayani humo hivyo ametoa wito wa kujitokeza kwa wingi kuja kwasikiliza.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria