Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
BAADA ya vipengele mbalimbali vilivyoboreshwa kwenye rasimu ya katiba mpya ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kupitishwa na wanachama na kuipa uwezo wa kusajiliwa, sasa ni rasmi katiba hiyo ndiyo itakayotumika katika uchaguzi mkuu ujao wa RT unaotarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia sasa.
Katika mkutano Mkuu uliofanyika leo kupitisha rasimu hiyo, ulitumia zaidi ya saa sita kujadili hadi kupitisha ajenda ya kupunguza idadi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kutoka watatu na kubakia mmoja.
Katika ajenda hiyo, uliibua mvutano kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 11:38 jioni ambapo wajumbe wakaridhia kipengere hicho ikiwa ni baada ya rais wa RT, Anthony Mtaka kuongea kwa hisia na kubadili ‘upepo’ wa msimamo wa wajumbe kwenye mkutano huo.
Kabla ya Mtaka kubadili muelekeo wa wajumbe, Kaimu msajili wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Ally Mchungahela aliingia kwenye mabishano na wajumbe hao akiwaeleza kuwa mabadiliko ya katiba hiyo ni kwa maslahi ya Taifa.
Wajumbe hao walimtaka kutoa ufafanuzi ni sheria ipi inaelekeza hivyo kabla ya Mchungahela kusisitiza sera ya michezo ndivyo inaelekeza kuwa na muundo huo.
Baada ya majibizano hayo na baadhi ya wajumbe, ilitokea kutosikilizana kwa dakika kadhaa kabla ya Mtaka kuzungumza kauli ambazo ziliwatuliza wajumbe huku akisisitiza RT inataka ufanisi wa riadha na si vinginevyo.
Kabla ya wajumbe kuridhia kuwa na mjumbe mmoja kutoka kila Mkoa kwenye Mkutano Mkuu na Uchaguzi Mkuu, mmoja wa wajumbe wa mkutano huo na mwanariadha nyota wa zamani, Gidamis Shahanga aliwahoji wenzake sababu za kung’ang’ania wajumbe watatu na wao wanaongoza vyama vya Mikoa kwa maslahi ya nani?.
Hoja hiyo ya Shahanga iligongelewa msumari na makamu wa pili wa rais wa RT, Ufundi, Dk Hamad Ndee ambaye aliwauliza wajumbe na mmoja kueleza kwamba kwenye uchaguzi mkuu, M wenyekiti wa Mkoa anaweza kuwa na maslahi binafsi, hivyo Mkoa ukitoa wapiga kura watatu itasaidia kuondoa urasimu, jambo ambalo Kamati Tendaji ya RT ilipinga huku ikiwahoji viongozi wa Mikoa kwa kutoaminiana.
Hata hivyo, msimamo wa wajumbe ulilegezwa na Mtaka aliyewaambia kuwa, Shirikisho linahitaji ufanisi wa mchezo huo na ndiyo sababu limelazimika kuwa na muundo huo kwenye rasimu ya Katiba.
“Kama tunahitaji ufanisi, lazima tukubali mabadiliko, twende kwenye muundo huu na RT itatumia fedha nyingine kusapoti timu za Mikoa,” amesema Mtaka kabla ya wajumbe kuridhia kupitisha kipengere hicho na kuendelea kujadili vipengere vingine vilivyofanyiwa mabadiliko ikiwamo cha kuajili Katibu Mkuu na RT kuwa na Bodi ya wadhamini ambavyo vote zilipitishwa.
Itakumbukwa kuwa, wakati Kamati ya marekebisho ya Katiba ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) ilipokuwa inakabidhi rasimu ya mabadiliko hayo kwa aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, ilipendekeza kupunguza idadi ya wajumbe wanaowakilisha Mkoa katika Mkutano Mkuu wa RT ambapo hadi sasa kila Mkoa unatoa wajumbe watatu ambao wote walikuwa wakipiga kura hivyo wanapendekeza mjumbe awe mmoja.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Filbert Bayi alisema kuwa, hata katika Shirikisho na Riadha la Kimataifa (WA) kila nchi inawakilishwa na mjumbe mmoja ambaye ndiye anayepiga kura ya uwakilishi hivyo mabadiliko hayo yatasaidia kupunguza gharama za uendeshaji.
Lakini pia mapendekezo mengine katika rasimu hiyo yaligusa kiwango cha elimu ambapo imependekeza wenye elimu angalau kuanzia Diploma kugombea nafasi ya Rais na Makamu huku ukomo wa kugombea ukiwa ni miaka 70 badala ya mihula.
Muundo wa Kamati Tendaji ya RT ambako hivi sasa itakuwa na Rais, Makamu wa Rais mmoja badala ya wawili, Katibu na Mweka Hazina wa kuajiriwa na Wajumbe sita wa Kamati Tendaji watakaotokana na Kanda pamoja na kuundwa kwa Kamati ya Nidhamu, Kamati ya Rufaa ya Nidhamu, Kamati ya Uchaguzi na Bodi ya Wadhamini.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania