Na Daudi Magesa, TimesMajira Online, Mwanza
MKURUGENZI wa Kampuni ya Mnengele & Associates,Arnold Herman Temba na aliyekuwa Meneja Uhasibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Mwanza, Josephat Jiroli wamepandishwa kizimbani mwishoni mwa wiki kwa makosa ya uhujumu uchumi.
Washitakiwa hao wanafanya idadi ya washitakiwa katika kesi namba 10 ya 2020 inayowakabili watu 7 waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Wakili wa Kujitegemea kufikia 10 ambapo awali washtakiwa wanane walisomewa mashitaka Juni 12, mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi Boniveture Lema.
Wakili Temba na Jiroli wamesomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Mwanza, Monica Ndiekobola ambapo wanakabiliwa na makosa ya kuongoza genge la uhalifu, wizi, utakatishaji fedha, kughushi na kutoa nyaraka za uongo na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 8.3 kinyume cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2006.
Walisomewa mashitaka na Waendesha Mashitaka wakiongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Yamiko Mlakano akisaidiwa na Waendesha Mashitaka wa Dorothea Kinyontho na Dismas Muganyizi.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka Joroli na Temba wanakabiliwa na makosa ya utakatishaji fedha ambayo ni kinyume na sheria ya uhujumu uchumi ambapo kati shitaka la 93 walidaiwa kwa nyakati tofauti wakishirikiana na watuhumiwa wa kwanza hadi wa nane kwa makusudi walikula njama kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 7.1.
Aidha katika shtaka la 94 washitakiwa hao kwa pamoja kati ya Julai 2019 na Januari 2020 waliisahabishia serikali hasara ya sh. milioni 417 pia katika shitaka la 95 kati ya Machi 2019 na Februari 2020 waliisababishia TPA hasara ya sh. milioni 848.6
Kutokana na upelelezi kutokamilika na kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi, Hakimu Ndiekobola ameahirisha hadi Julai 9, mwaka huu itakapotajwa tena na hivyo washitakiwa wote walirudishwa mahabusu.
Katika kesi hiyo mshitakiwa wa kwanza ni Deogratius Lema ambaye alikuwa Mhasibu Mwandamizi wa TPA Makao Makuu, wa pili ni Aike Mapuli (pia alikuwa Mhasibu Mwandamizi wa TPA Makao Makuu), Marystella Minja (Afisa Uhasibu Makao Makuu), Thomas Akile (Mhasibu Kituo cha TPA Mwanza) na Ibarimu Bunyoga (Mhasibu Msaidizi TPA, Mwanza).
Wengine ni Wendellin Tibuhwa (Keshia TPA), James Mbedule (Afisa Kodi TPA, Mwanza ), Leocard Kipengele, wakili wa kujitegemea kutoka kampuni ya Mnengele & Associates na ELA advocates, Josephat Jiroli aliyekuwa Meneja Uhasibu TPA Mwanza na Wakili Arnold Herman Temba, Mkurugenzi wa Mnengele & Associates.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi