Na Esther Macha,Timesmajira,Online, Mbeya
MFANYABIASHARA na mkurugenzi wa Kampuni ya Giant Tanzania Printers Ltd iliyopo Jijini Dar es Salaam aitwaye Deogratius Magubo amefariki dunia akiwa amelala nyumba ya wageni iitwayo DICCO INN iliyopo maeneo ya Iyunga mkoani Mbeya .
Kamanda wa polisi Mkoani Mbeya , Benjamin Kuzaga amesema kuwa tukio hilo limetokea juni ,19 mwaka huu majira ya saa 9.00 usiku ambapo marehemu alifika katika nyumba hiyo ya kulala wageni iitwayo DICCO INN iliyopo eneo la Iyunga akiwa ametokea Jijini Dar es Salaam na kuingia kwenye chumba namba 208 na hivyo umaiti kumkuta.
Kuzaga amesema kuwa taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa kampuni ya “Giant Tanzania Printers Ltd” akiwa amelala katika nyumba ya kulala wageni iitwayo DICCO INN iliyopo maeneo ya Iyunga mkoani Mbeya kwamba sio cha kawaida.
Aidha Kamanda wa Polisi mkoani hapa Benjamin Kuzaga amesema kuwa Juni 21,mwaka huu majira ya saa 5:40 asubuhi, zilipokelewa taarifa katika kituo kikuu cha Polisi Mbeya (Central Police Station) kutoka kwa Meneja wa nyumba hiyo ya kulala wageni kwamba huko katika nyumba ya kulala wageni iitwayo DICCO INN katika chumba namba 208 kuna mteja aliyetambulika kwa jina la Deogratius Magubo hajaamka mpaka muda huo.
Amesema baada ya taarifa hizo timu ya makacher wa Jeshi la Polisi ikiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Mbeya akiwa na kiongozi wa Mtaa huo ilifika eneo la tukio na kuanza kugonga mlango bila mafanikio yoyote hivyo kulazimika kuvunja mlango wa chumba hicho uliokuwa umefungwa kwa ndani na kumkuta Deogratius Magubo akiwa amefariki dunia akiwa amelala kitandani .
Hata hivyo uchunguzi uliofanyika katika chumba hicho mbele ya kiongozi wa Mtaa ulikuta dawa mbalimbali za binadamu, Haloxen 1.5, Haloperidol Injection BP, Valparin Chrono 500, Cough Mixer Syrup pamoja na chupa tupu ya pombe aina ya Grants 750ml, Glass ndani yake ikiwa na vipande vitatu vya limao. Katika uchunguzi huo uliofanywa na jeshi la Polisi katika chumba alichokuwa amepanga marehemu umebaini kuwa hakuna kitu kingine kinachotiliwa mashaka.
Akielezea zaidi Kamanda Kuzaga amesema kuwa juni 24, mwaka huu mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na Daktari Mtaalamu wa Upasuaji (Pathologist) wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya mbele ya ndugu wa marehemu na kuchukua sampuli za mwili wa marehemu na kutumwa kwa wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi.
Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya linasubiri matokeo ya uchunguzi na majibu ya Wakala wa Mkemi Mkuu wa Serikali kulinganisha na majibu ya Daktari Mtaalamu wa Upasuaji (Pathologist) ili kuthibitisha kifo cha Deogratius magubo ikilinganishwa na uchunguzi wa awali uliopatikana kwenye chumba alichokuwa amepanga.
Aidha jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa mtu yeyote mwenye ushahidi mwingine mbali na ushahidi wa kisayansi uliokusanywa asisite kuuwasilisha badala ya kuendekeza taarifa za hisia kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato