January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Msalala asisitiza haki, uadilifu

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

WATENDAJI wote wa Halmahauri ya Msalala, Kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuwa waadilifu na kutenda haki kwa wananchi wote wanaowahudumia, ili kujenga imani na serikali iliyopo madarakani.

Akizungumza katika semina iliyolenga kutoa mafunzo kwa watendaji wao ili kuboresha utendaji kazi wao, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Khamis Katimba alisema, utumishi wenye weledi na ufanisi mkubwa utapunguza kero kwa wananchi.

Mafunzo hayo yaliyohusisha Watendaji wa Kata 18 na Watendaji wa Vijiji 92, yalitokana na maelekezo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa aliyeaguzi wakurugenzi wote kuwapa mafunzo mbalimbali watumishi ili kuwaongezea ujuzi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Akifungua mafunzo hayo, Katimba aliwashauri watumishi hao kuwashauri vizuri viongozi waliopo katika maeneo yao ya kazi na kuwasimamia watumishi waliopo katika kata na vijiji vyao.

“Masuala haya yote yatawezekana iwapo watendaji mtakuwa mfano kwa watumishi wengine ikiwa ni pamoja na kufika ofisini kwa wakati na kutoka saa 9.30 alasiri, lakini pia kutumia lugha yenye staha kwa wateja wanaokuja kupata huduma katika ofisi zenu.

“Nakutana nanyi mara kwa mara lengo langu kubwa ni kuhakikisha mnaweza kujiendesha wenyewe na kuwaza nini utaifanyia halmashauri yako na nchi yako kwa ujumla,” alisema.

Alisema, halmashauri hiyo inatumia gharama kubwa ili kuhakikisha watumushi hao wanasimama imara na kuwa nguzo muhimu ya utatuzi wa changamoto za wananchi.

“Simamieni mapato na kuhakikisha fedha za serikali zinakusanywa. Ndio maana watendaji wa kata wote nimewapa pikipiki.

“Fanyeni ziara za kushtukiza ndani ya vijiji ili kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wengine, nami nitapita kuona hili kama linatekelezwa na pale nitapoona kuna uzembe, nitachukua hatua,” alisema.

Kwenye mafunzo hayo, miongoni mwa mada zilizowasilishwa ni majukumu ya Mtendaji wa Kata na Kijiji, vikao vya kisheria vinavyopaswa kufanywa ngazi ya kijiji na kata, chimbuko la Mamlaka za Serikali za Mitaa na sababu za kuanzishwa kwake.

Pia dhana nzima ya utawala bora, ukusanyaji mapato na sababu za msingi za kisheria za kwa nini Mamlaka za Serikali za Mitaa zikusanye mapato, masuala ya TASAF na fursa zijazo kwa ajili ya machinga.

Mada hizo ziliwasilishwa na Mwanasheria wa Halmashauri hiyo, Leonard Mabula akishirikiana na Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimazi wa Rasilimali Watu, Mary Nziku ambaye amewataka watendaji hao kuthamini nafasi walizonazo na kuzitumikia kwa bidii ili kuleta tija ndani ya halmashauri hiyo.

Baadhi ya watendaji hao wamepongeza hatua ya halmashauri hiyo kukutana nao mara kwa mara katika jitihada za kuhakkikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi.

“Hongera sana kiongozi wetu (mkurugenzi) nasi hatutakuangusha,” alisema Patrick Mahona, Mtendaji wa Kata ya Segese, Msalala.

Neema Magwega, Mtendaji wa Kijiji cha Ntambalale ameishukuru halmashauri kwa kutoa mafunzo kwa mabaraza ya ardhi ya kata ili kukabiliana na migogoro ya ardhi.